31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri azungumzia upungufu dawa za wajawazito

MWANDISHI WETUDAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amezungumzia taarifa ya kuwapo upungufu wa dawa za wajawazito katika baadhi ya wilaya mkoani Kagera, huku akiwataka waganga wa wilaya na mkoa kutoa taarifa hiyo kwa haraka.

Kauli hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Health Promotion Tanzania (HDT) kutoa taarifa kuhusu kukosekana kwa dawa muhimu na hatari ya kuongezeka vifo vya mama na mtoto baada ya kujifungua.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ummy alisema hajaiona taarifa ya HDT, lakini pamoja na kuwapo kwa baadhi ya changamoto, bado dawa muhimu zinapatikana katika vituo vya kutoa huduma za afya.

“Sijaiona hiyo ripoti (ya HDT), ila dawa muhimu zinapatikana katika vituo vya kutoa huduma. Kama huko Kagera kuna changamoto, basi ni bora ucheki na Mganga Mkuu wa Mkoa wakueleze tatizo ni nini.

“Katika mikoa na wilaya nyingi nchini hali ya upatikanaji wa dawa muhimu ni nzuri. Changamoto yetu kubwa sasa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila ya kikwazo cha fedha. Hili litawezekana endapo wananchi watajiunga na mifuko ya bima ya afya,” alisema Ummy.

Akizungumza hivi karibuni Dar es Salaam kuhusu hali ya upungufu wa dawa muhimu kwa mama wajawazito katika baadhi ya vituo vya afya, Mkurugenzi Mtendaji wa HDT, Dk. Peter Bujari, alisema asilimia 68 ya vifo vya wajawazito vinatokana na sababu zinazozuilika.

Dk. Bujari alizitaja sababu hizo kuwa ni kifafa cha mimba, kupoteza damu wakati na baada ya kujifungua na upungufu wa damu wakati wa ujauzito.

Alizitaja dawa muhimu ambazo zinaweza kuokoa maisha ya wajawazito ni Ferrous Sulphate, Misoprostol na Oxytocin.

“Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, zinaonesha kwamba tangu mwaka 2000 hadi 2005 vifo vitokanavyo na uzazi havijapungua sana.

“Hata hivyo, pia vimekuwa vikipanda na kushuka.

“Sasa ni lazima mamlaka za Serikali ziamue na kusimama kidete ili kufuatilia kwa kina hili suala la upatikanaji wa dawa muhimu,” alisema Dk. Bujari.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wao walioufanya vituo vya afya vya Nyakahura, Ngarambe, Kalege na Lusange wilayani Biharamulo mkoani Kagera, bado kuna changamoto ya upungufu wa dawa na hata baadhi kukosekana kabisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles