WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema wanafunzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanaosoma vyuo vikuu wamekuwa wakifuata taratibu katika mikutano yao tofauti na wanafunzi wanaotokea Chama cha Demorasia na Maendeleo (Chadema).
Hayo aliyaeleza jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (Chadema).
Msigwa alidai wanachama wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kutoka Chadema (Chaso) wanazuiwa kufanya mikutano wakati wenzao wa CCM wakiruhusiwa.
‘’Unawezaje kusema Demokrasia tunafanya kwa kiwango kikubwa wakati kuna upendeleo wa waziwazi ni sawa na katika ndondi mmoja amefungwa mikono halafu unasema upigane.
‘’Je, waziri atakuwa tayari kuliagiza Jeshi la Polisi liache upendeleo katika kutekeleza majukumu yake ya Kupractise Demokrasia,’’ aliuliza Msigwa.
Akijibu swali hilo, Mwigulu alisema katika kufanya mikutano kuna taratibu ambazo zinatakiwa zifuatwe kabla ya kuomba kufanya mkutano wowote.
‘’Kuhusu mikutano taratibu zipo wazi kama CCM wamefuata taratibu na wengine wanatakiwa kufuata taratibu zilezile waweze kupewa mkutano.
‘’Lakini wengine kama hawajafanya utaratibu hawatapewa na hawezi kupewa tu kwa sababu CCM walipewa watapewa kwa kufuata utaratibu na tumekuwa tukifanya kote.
‘’Mbona kuna sehemu nyingine Chaso hao hao wamepewa nafasi ya kufanya mikutano kwa hiyo kinachotakiwa ni kufuata utaratibu wa kupewa mikutano hiyo,’’ alisema.