22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 1, 2022

Waziri awaachia neno gumu wafanyabiashara wa madini

 

Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA

WAFANYABIASHARA wa madini (Dealers), wametakiwa kutembelea Gereza la Kisongo jijini hapa kusaidia wafungwa na mahabusu maji kwani hawajui nini kitafuata miongoni mwao.

Kauli hiyo ilitolewa jijini hapa hivi karibuni na Waziri wa Madini, Angela Kairuki, alipofanya mazungumzo ya kina na Chama cha Mawakala wa Madini Tanzania (TAMIDA).

Akizungumza na wanachama hao, Waziri Kairuki aliwataka kuanza kujitafakari upya kwa waliokuwa hawalipi kodi na kushiriki mbinu za utoroshaji madini kwani hawapo salama.

“Kabla ya kushiriki kutorosha madini jitafakari upya, unaipenda familia na wanaokutegemea? Ningeomba muanze kulitembelea Gereza la Kisongo kawasaidia maji wafungwa kwa sababu hamjui nini kitafuata kwenu.

“Ninasema haya si kwamba nawatisha, napenda sana muwe na mafanikio katika biashara hii, lakini kwa kufuata sheria na taratibu za nchi. Haitapendeza siku moja unajikuta umepata kosa la uhujumu uchumi.

“Siwatishi, mimi ni mama na dada yenu, ninawapa ushauri tusifike huko, tamaa ya muda mfupi itagharimu na kuleta athari kwa familia zenu na wanaowategemea,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanafuata na kutekeleza kila kilichopo kwenye leseni zao, ikiwamo kusoma na kuzifanyia kazi sheria za madini.

“Tutaendelea kufanya marekebisho ya sheria ili ziwe kali zaidi. Niwaombe hakikisheni mnasafisha nyumba yenu na kuanzia sasa tukubali kubatizana upya na kufungua ukurasa mwingine,” alisema Waziri Kairuki.

Kwa upande wake, mwekezaji wa Kampuni ya Tanzania One inayofanya kazi kwa ubia na Serikali kupitia Shirika la Madini (Stamico), Faisal Juma, alisema watahakikisha taifa linanufaika na biashara wanayoifanya.

“Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri tupo tayari kufanya kazi na kuona taifa likinufaika. Tunajua wakati huu si wa kulumbana na Serikali,” alisema Juma.

Naye Mwenyekiti wa Tamida, Sam Mollel, akizungumza wakati wa kikao kazi hicho kilichowakutanisha wafanyabiashara takribani 55, aliwataka kuanzia sasa kujipanga kuongeza thamani ya madini yao hapa nchini.

“Ndugu zangu hii ndiyo dira ya Serikali yetu, tujipange kuongeza thamani ya madini kwa kununua mashine na kuleta wataalamu ili pia wawafundishe wazawa kufanya kazi hizo,” alisema Mollel.

Aidha Waziri Kairuki alifanya ziara katika mpaka na nchi jirani ya Kenya uliopo Namanga wilayani Longido kujionea kazi zinazofanywa na maofisa wa wizara yake katika kukabiliana na utoroshaji wa madini.

Mwisho.

 

Lugola kupambana na polisi walarushwa

Na Felix Mwagara – Mwibara

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema hatawaonea huruma polisi watakaokamatwa wakichukua rushwa na wale wanaonyanyasa wenye magari, bodaboda na wananchi.

Lugola ambaye ni mbunge wa Mwibara, alisema anapokea taarifa mbalimbali zikilalamikia tabia za baadhi ya polisi kuwaonea wananchi wasio na makosa kwa kutumia nguvu na kuwalazimisha kuwaweka mahabusu hata kama kosa halistahili kuwekwa ndani.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Victoria, Mji mdogo wa Kisorya, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, jana, Lugola alisema atahakikisha anapambana na askari ambao wamechoka kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

“Serikali ya awamu ya tano si ya mchezo mchezo, nawahakikishia wananchi wa hapa Kata ya Nansimo na pamoja na kote nchini, mimi Lugola sitamwangusha mheshimwa Rais Magufuli, sitawaangusha nyie wananchi, ninawaahidi hii tabia nawahakikishia kwa mara nyingine nitaimaliza,” alisema Lugola huku akishangiliwa.

Aliongeza kuwa magari na bodaboda ambazo hazina makosa, hazipaswi kubughudhiwa kwa sababu wamefuata taratibu zote za usalama barabarani.

“Kitendo cha askari akiwa na masilahi yake binafsi au ametumwa na mtu mwenye masilahi naye kwenda kukamata gari fulani au bodaboda kwa lengo la kujipatia rushwa tabia hiyo inapaswa kulaaniwa.

“Muda mwingine utakuta mwananchi mmoja ambaye ana masilahi na polisi anakamata gari au bodaboda yake na mmiliki wa chombo hicho cha moto huwekwa mahabusu na ukiuliza ‘nimefanya kosa gani’ wanakujibu ‘kaa ndani kwanza’, na ukiingia bure, lakini wanapokutoa unawapa rushwa, nalijua hilo vizuri sana, tabia hii haivumiliki, na nitahakikisha wananchi wa jimbo hili pamoja na Tanzania nzima mtakuwa salama,” alisema Lugola.

Alifafanua kuwa kuna baadhi ya polisi uwaweka mahabusu wananchi hovyo ili kuwatisha kwa lengo la kujipatia rushwa.

“Si kila kosa mwananchi awekwe mahabusu, yapo makosa ambayo polisi wanaweka mahabusu wananchi kwa mujibu wa sheria, lakini kitendo cha askari kumkamata mwendesha bodaboda akimlazimisha atoe rushwa au awekwe mahabusu hilo halitakubalika,” alisema.

Pia alisema wananchi wanapoonewa mara kwa mara kunatengeneza chuki dhidi ya Serikali, kwa sababu wanastahili kuishi katika mazingira ya amani na utulivu, hivyo tabia ya baadhi ya askari hao haiwezi kuvumilika.

“Hii tabia ya baadhi ya askari wanasema ‘injika ugali mke wangu mboga inakuja’ akielekea barabarani au mahali popote na kuanza kutafuta rushwa kwa nguvu zote kwa wenye magari, bodaboda au mazingira yoyote.

“Mimi Kangi Lugola naapa nitaisambaratisha haraka iwezekanavyo tabia hii, sitakuwa na huruma katika hilo na nitakuwa nafanya ziara ya kushtukiza ili niwakamate hao wenye tabia hiyo chafu katika nchi yetu,” alisema Lugola.

Hata hivyo, Lugola aliwataka polisi nchini kuwakamata waendesha magari na bodaboda ambao hawafuati sheria za barabarani.

Alitoa mfano baadhi ya waendesha bodaboda wanaovunja sheria kwa makusudi kwa kupakia abiria zaidi ya wane, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa dereva na abiria wake.

“Polisi wangu wengi wanafanya kazi kwa umakini na uaminifu mkubwa, ila wachache sana ndio wenye tabia hizo mbaya, nawataka askari hao wafuate sheria na pia kuendelea kuzikamata kama ni magari au bodaboda au wananchi wowote ambao wanavunja sheria za nchi,” alisema Lugola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,373FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles