23 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

WAZIRI ATOA TAHADHARI  UPIMAJI DNA

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM


NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee  na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema upimaji wa vinasaba nchini (DNA), unapaswa kufuata sheria na kuitaka jamii kuacha kuamrisha Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kupima watu bila kufuata taratibu.

Dk. Ndugulile alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi ya kwanza ya GCLA, inayoongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Esther Jason, aliyeteuliwa Desemba mwaka jana, akiwa na wajumbe saba  kati ya tisa wanaopaswa kuwapo kwa mujibu wa sheria, walioteuliwa Februari mwaka huu.

Alisema kuna haja ya ofisi hiyo kuanza kutoa elimu kwa jamii ili kujua taratibu za kufuata endapo mtu atahitaji kuchukuliwa sampuli ama kutaka mtu achukuliwe sampuli za kupima DNA kwa mujibu wa sheria.

“Hivi karibuni kulitokea vurugu kuhusu upimaji wa DNA, kwa sababu hiyo, sasa naona ipo haja ya wakala kutoa elimu kwa jamii, kuwaelimisha taratibu na sababu za wahusika kupima DNA, wanapaswa kufahamu si kila mtu anaamrisha mamlaka kwa kumwambia mkemia mkuu kuchukua vipimo, tufuate taratibu,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema suala la upimaji wa DNA lipo kisheria na mara zote majibu yanayotolewa na ofisi hiyo hutumika kama kielelezo katika masuala mbalimbali zikiwamo kesi, hivyo endapo vipimo vitachukuliwa kiholela, vinaweza vikasababisha kesi kufutwa.

Mbali na hilo, pia ameitaka ofisi hiyo, kuangalia matumizi ya kemikali zinazoingizwa nchini kwakuwa kwa sasa zinatumika kinyume na taratibu, ikiwamo kutengeneza dawa za kulevya.

“Kuna changamoto kubwa ya matumizi ya kemikali, zinaingia ovyo na kutumika ovyo, lazima tudhibiti kila mkono na kila tone la kemikali linaloingia nchini, lazima tujue linatoka wapi na linatumika kwa matumizi gani,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema wapo waagizaji wa kemikali ambao si waaminifu, wanatumia bidhaa hizo kutengeneza mabomu, huku wengine wakitumia kemikali bashirifu kutengeneza dawa za kulevya.

Awali Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, alisema pamoja na ofisi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha, kumekuwa na changamoto ya watumishi na kwa sasa kuna upungufu wa wafanyakazi 117 kati ya 400 wanaohitajika.

“Kwa sasa mamlaka ina jumla ya watumishi 228, kati ya hao 117 ni wataalamu na 111 ni wa kada zinazosaidia uendeshaji wa taasisi, idadi hiyo inafanya tuwe na upungufu wa watumishi 117 kati ya 400 wanaohitajika,” alisema Dk. Mafumiko.

Alisema mamlaka tayari imeshaomba kibali cha kuajiri watumishi hao ili kuweza kuondoa changamoto hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,305FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles