Na MWANDISHI WETU-GEITA
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita kufungua duka la dawa ili kutoa huduma karibu na wananchi na kuongeza mapato ya hospitali.
Waziri Ummy alitoa agizo hilo jana alipoitembelea hospitali hiyo ili kuona hali ya miundombinu pamoja na utoaji wa huduma za afya.
“Tumeshaagiza hospitali zote nchi nzima kuwa na maduka ya dawa, kwa nini hapa hamjafungua duka lenu?,” alihoji na kuongeza. “Sasa nawapa miezi miwili uongozi wa hospitali kuhakikisha mnafungua duka la dawa la hospitali ili liweze kuwasaidia kupandisha mapato lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisisitiza waziri huyo.
Pamoja na hayo Waziri Ummy lieleza kuridhishwa na upatikanaji wa dawa kwa zaidi ya asilimia 90 na uboreshwaji wa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Awali Waziri Ummy alitembelea ujenzi wa Hospitali Teule ya Mkoa wa Geita ambapo alishuhudia ujenzi huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 54, lakini amemtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi huo ambaye ni wakala wa ujenzi (TBA) kufanya kazi usiku na mchana ili hospitali hiyo ianze kufanya kazi ifikapo Julai mwaka huu.
Waziri huyo alikamilisha ziara yake kwa kutembelea pia Hospitali ya Wilaya ya Chato mkoani humo kujiridhisha na utoaji wa huduma za afya na miundombinu pamoja na kuhakikisha kama vifaa na vifaa tiba vinapatikana kwa urahisi.