30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

WAZIRI ATAKA WACHIMBAJI WADOGO WAZINGATIE SHERIA

Na Mohamed Saif


WACHIMBAJI wadogo wa madini nchini wametakiwa kufanya shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia sheria, kanuni za usalama migodini kuepusha ajali.

Wito huo ulitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alipozungumza na wachimbaji wadogo wa   dhahabu kwenye mgodi wa Musasa uliopo Kata ya Makurugusi wilayani Chato.

Alisema njia bora ya kuepukana na ajali migodini ni kufanya shughuli za uchimbaji kwa kutii sheria za uchimbaji madini bila shuruti.

Aliwaasa pia kuzingatia kanuni za usalama kwenye maeneo ya machimbo na wakati wa shughuli za uchimbaji.

Naibu Waziri alisema  wachimbaji wadogo wa madini kote nchini hawana budi kujifunza kutokana na ajali mbalimbali zinazotokea migodini.

  Dk. Kalemani aliwasisitiza wachimbaji wa madini   nchini kuhakikisha wanafanya shughuli za uchimbaji kwa kutunza mazingira na afya zao pamoja na afya za wengine wanaozunguka machimbo husika.

Alisema suala la mazingira linapaswa kupewa kipaumbele wakati wa shughuli husika.

“Ni jukumu la kila mchimbaji na kila anayeishi au kufanyia shughuli zake maeneo ya machimbo kuhakikisha anaboresha mazingira   kuepusha majanga mbalimbali yakiwemo  magonjwa ya mlipuko.

“Chimbeni madini kwa kutunza mazingira na afya zenu ili mpate kufaidi matunda yanayotokana na shughuli hii,” alisema Dk. Kalemani.

  Naibu waziri pia  aliwakumbusha wachimbaji wadogo wa madini kulipa kodi na ushuru stahiki  kuepuka usumbufu.

Aliwahakikishia wachimbaji wadogo wa madini watafanya shughuli zao bila kubughudhiwa endapo watafuata maelekezo ya sheria.

“Mkitaka kuishi salama na kufanya shughuli zenu bila kubughudhiwa, hakikisheni mnalipa kodi na tozo mbalimbali mnazopaswa kulipa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles