29.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 19, 2022

Waziri ataka halmashauri kukusanya Sh bilioni 1.9 inayodai taasisi za umma

Mwandishi wetu, Kilombero

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula, ameiagiza halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro kuzifuatilia taasisi za Serikali zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi kwenye halmashauri hiyo zaidi ya bilioni 1.9 ili ziweze kulipa deni hilo.

 Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana alipokutana na uongozi wa Wilaya ya Kilombero na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za Wilaya ya Kilombero na ile ya Ifakara wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro.

 Agizo la Dk Mabula linafuatia kuelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Injinia Stephano Kaliwa, kuwa miongoni mwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika halmashauri yake ni taasisi za Serikali zinazodaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.9.

 Alizitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linalodaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.7 katika maeneo yake inayomiliki ya Kidatu Sh 1,007,452.00, Kihansi  Sh996,957,750.00 na Mlimba Sh 29,826,650.00 huku taasisi ya The Trustees of TANAPA nayo inadaiwa jumla ya Sh 12,819,550.00.

 Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Remigi Lipiki, alimueleza Mabula kuwa, TANESCO imetaka kufanyika uhakiki kwanza wa deni lake kwa madai kuwa baadhi ya maeneo inayomiliki yalishachukuliwa na taasisi nyingine na kutolea  mfano wa eneo la Kidatu. 

  Alisema pia wanapata changamoto ya ukusanyaji kodi ya ya ardhi kwa baadhi ya wawekezaji wa mashamba kutokana na kutokamilika taratibu za uhaulishaji mashamba ambayo wamiliki wake hawana nyaraka.

 Aliataja baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo kuwa ni Kampuni ya Mufindi Paper Mills yenye hekta 10,000 , Green Resource Limited hekta 25,000, Hiragro Ltd hekta 1500 na Sygen yenye ekari 30,000. 

Kwa mujibu wa Kaliwa, kutokana na kutokamilika mchakato wa uhaulishaji wa mashamba hayo kumekuwa na upotevu wa makusanyo ya kodi ya Sh 132,865,031.00 kila mwaka.

 Dk Mabula akizungumzia suala la pango la ardhi kwa taasisi za umma, alisema alisema, halmashauri ya Wilaya ya Kilombero lazima ihakikishe inazifuatilia taasisi hizo ili ziweze kulipa madeni ya kodi ya ardhi kwa kuwa taasisi hizo zimekuwa zikitenga fedha kwa ajili ya malipo ya huduma mbalimbali ikiwemo kodi hiyo ya pango la ardhi.

“Taasisi zinashindwa kulipa madeni na hazijachukuliwa hatua, haiwezekani deni lifikie zaidi ya bilioni moja, fuatilieni suala hili na mchukue hatua za kisheria,’’ alisema Dk Mabula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,987FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles