23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Waziri amsweka lokapu mkandarasi

DERICK MILTON-MASWA

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, ameagiza kukamatwa na kuwekwa lokapu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ukandarasi PET Cooperation, Tryphone Elias, kwa kushindwa kukamilisha mradi wa chujio la maji kwa muda.

Mradi huo ulioko katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, unagharimu kiasi cha Sh bilioni 3.5, ambapo ulitakiwa kujengwa kwa muda wa miezi nane lakini umetimiza miaka minne toka 2015 bila ya kukamilika ujezi wake.

Waziri Mbarawa, alionekana kukasirishwa na hali hiyo mara baada ya kufanya ziara ya ghafla juzi saa 1:00 jioni ya kukagua mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 92 kabla ya kukamilika kwake.

Baada ya kupata maelezo ya mradi huo, Waziri Mbarawa, aliagiza mkurugenzi wa kampuni hiyo kuwekwa mahabusu kwa muda wa saa mbili, kisha kuandika maelezo ya kuhakikisha anakamilisha mradi ndani ya siku 11.

Kabla ya kutoa maagizo hayo, Waziri huyo alisema mkadarasi huyo amepewa miradi 15 kwenye maeneo mbalimbali nchini, ambayo yote imeshindwa kukamilika kwa wakati.

Prof. Mbarawa, alimtuhumu Mkurugenzi huyo kutumia njia za rushwa kupewa miradi hiyo akisisitiza kuwa: “Haiwezekani miradi yote 15 mtu mmoja na yote imemshinda, hakuna mradi ambao umekamilisha ujenzi wake, umeendelea kukatili wakazi wa mji wa Maswa kutumia maji yenye tope.

“OCD, Mkuu wa Wilaya naomba usimamie hili, akamatwe sasa hivi awekwe lokapu saa mbili, huo muda ukiisha aandike maelezo ndani ya siku 11 awe amekamilisha akishindwa kuandika hayo maelezo vizuri hakuna kutoka,” aliongeza Waziri Mbarawa.

Mbali na kumpa muda wa siku 11 kuanzia jana awe amekamilisha kazi zilizobaki, Waziri huyo alisema ikiwa atashindwa kwa muda huo atavunja mkataba ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani kwa utapeli.

“Tayari nimesaini kiasi cha Sh milioni 152.23, ili alipwe mkandarasi huyu na Jumatano wiki ijayo pesa zote zinatoka, asipokamilisha tunavunja mkataba na kukupeleka mahakamani maana huo utakuwa utapeli,” alisema Waziri.

Awali akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Salama Mji wa Maswa (MAUWASA), Mhandisi Merchades Anaclet, ambao ndio wasimamizi wa mradi, alisema tatizo kwa mkadarasi huyo ni kasi ndogo.

Alisema wamekaa na mkandarasi huyo zaidi ya vikao sita kujua ni lini atakamilisha mradi huo, lakini alieleza kila anapotoa tarehe ya kukamilisha amekuwa hafanyi kama alivyoahidi.

“Tulikuwa tunamkata fedha mara baada ya muda wa mkataba kuisha kama sheria inavyotaka, lakini tatizo limebaki pale pale kila siku anatoa tarehe ya kukamilisha lakini anashindwa, hatua ya mwisho tulikubaliana kuvunja mkataba,” alisema Anaclet.

Kwa upande wake Mkurugenzi huyo wa kampuni, Tryphone Elias, alisema tatizo la kuchelewa kumaliza mradi ni kutolipwa fedha kwa wakati pindi anapowasilisha hati za malipo kwa kazi anayoikamilisha.

“Jumla ya hati za malipo tatu zilichelewa kulipwa kwa zaidi ya miaka mitatu, hali hiyo imefanya baadhi ya vitu kupanda bei sokoni na kunilazimu nitumie fedha zangu kwa ajili ya kuongezea, ukweli napata hasara kutokana na fedha za malipo kuchelewa,” alisema Elias.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles