26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri ahimiza ubunifu kwa vijana

JANETH MUSHI-ARUSHA

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ,William Ole Nasha, amewataka vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali vya ufundi hapa nchini kuwa wabunifu na kuanzisha ajira binafsi na kusaidia jamii kupitia taaluma zao.

Ole Nasha aliyasema hayo jana jijini hapa, alipokuwa akizungumza katika mahafali ya 11 ya Chuo  cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo wahitimu 436 walitunukiwa  Astashahada , Stashahada, Shahada ya Juu na Shahada katika fani mbalimbali za ufundi.

Alisema vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali vya ufundi wanatakiwa kujikita kuanzisha ajira mpya badala ya kusubiri ajira chache zilizopo hivi sasa na kuwa wana uwezo wa kutumia taaluma zao kusaidia jamii kwa kuajiri wengine.

“Ni muhimu kuwa wathubutu na kuanzisha ajira zenu wenyewe na miradi midogo midogo kwani zitakua, badala ya kukaa majumbani na kusubiri ajira.

“Mafanikio katika maisha hayatategemea tu elimu mliyopata hapa bali yatachangiwa zaidi na nidhamu pamoja na uthubutu wa kujaribu, natambua ziko changamoto nyingi katika kujiajiri lakini ukiwa na nia na kuthubutu unaweza kwani fursa zipo nyingi katika ufundi,” alisema.

Alisema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa Elimu ya Ufundi Afrika Mashariki ambao unalenga kuvijengea uwezo vyuo vya ufundi ili viweze kuzalisha wahitimu wenye ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elisabeth Jacobsen, alisema Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha elimu ya ufundi ambayo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Naye Kaimu Mkuu wa ATC, Dk Masudi Senzia alisema kuwa chuo hicho kimeongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika masomo yake kutokana na idadi ndogo ya  vijana wa kike wanaojiunga na elimu ya ufundi.

Kaimu huyo aliiomba serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo iwezeshe ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike ambao asilimia kubwa wanaishi nje ya chuo.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ufundi  Arusha (ATC), Chacha Wambura,  alipongeza juhudi  zinazofanywa na serikali katika kuboresha elimu ya ufundi na kujenga miundombinu rafiki na vifaa vya kisasa vya kujifunzia suala linalochangia wahitimu kubobea katika fani zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles