25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aagiza kukatiwa umeme wanaodaiwa na Tanesco Simiyu

Na Derick Milton, Simiyu

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, amemtaka Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Simiyu, Alistidia Clemence, kutekeleza maagizo ya Wizara kwa wateja ambao wamekuwa sugu kulipa madeni ya huduma ya umeme.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa maagizo ya Wizara ni kuwakatia umeme wateja wenye madeni sugu, lakini kuwafuatilia mara baada ya kukatiwa huduma ili kuhakikisha wanalipa madeni hayo au kupunguza kiasi cha deni ambacho wanadaiwa.

Byabato ametoa maagizo hayo leo Jumatano Februari 24, 2021 wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo, ambapo amemtaka Meneja huyo kuwakatia huduma ya umeme wateja wote ambao wanadaiwa na Shirika hilo.

“Kuhusu suala la madeni kwa wateja wa Tanesco, kama Wizara tumekwisha kutoa maagizo, wale wote ambao wanadaiwa na Shirika wakatiwe huduma lakini pia wafuatiliwe kuhakikisha wanalipa au wanapunguza deni lao.

“Naagiza hapa Meneja Tanesco Mkoa, wale wote ambao mnawadai, wakatieni huduma kuanzia sasa, na mkawafuatilie kuhakikisha wanalipa deni hilo, hata kama kwa kupunguza tu, lakini tuwe na mwelekeo wa kuhakikisha wanalipa deni lote,” amesema Byabato.

Awali akisoma taarifa yake, Meneja wa Tanesco Mkoa, Clemence amesema kuwa Shirika hilo linadai kiasi cha zaidi ya Sh milioni 700 kutoka kwa wateja wakubwa, wa kati na kawaida ambapo kati ya wateja hao ni Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Wilaya ya Maswa (MAUWASA).

“Hadi kufikia Desemba 2020 Shirika lilikuwa linawadai wateja wake wakubwa, wa kati, na wadogo zaidi ya milioni 774, kati ya wateja hao ipo Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Maswa (MAUWASA) ambao tunawadai zaidi ya Sh milioni 100, na mteja mwingine tunamdai zaidi ya Sh milioni 400,” amesema Clemence.

Akizungumzia changamoto ya kukatika katika kwa umeme katika Mkoa huo, Byabato amesema kuwa Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ataweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha kupozea umeme Machi 3, 2021 ambacho kitakuwa suruhisho la changamoto hiyo.

“Tunategemea ujenzi wa kituo hicho unaenda kumaliza tatizo la kumaliza kukatika katika kwa umeme katika mkoa huu ambalo limekuwa kero, kituo hiki kitazalisha megawati 90 na matumizi ya mkoa ni megawati 10,” amesema Byabato.

Aidha, Byabato amesema kuwa jumla ya vijiji 183 ambavyo havijapata umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza, tutapata huduma hiyo katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao utekelezaji wake unaanza mwezi Februari, mwaka huu.

Naye Katibu Tawala Mkoa, Miriam Mmbanga, amesema kuwa changamoto ya kukatika katika kwa umeme katika mkoa huo, imesababisha baadhi ya wawekezaji kushindwa kwenda kuwekeza.

“Tumepata wawekezaji wengi hapa wa viwanda mbalimbali, lakini wakiangalia uwezo wetu kwenye Nishati ya umeme, wanabadilisha mawazo na kwenda kuwekeza kwingine, tatizo hili ni kubwa na tunaiomba serikali au Wizara kutusaidia kujegwa haraka kwa kituo cha kupozea umeme,” amesema Mmbaga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles