31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIMBABWE WAPIGA KURA, MNANGAGWA ADAIWA  KUMNYANG’ANYA MUGABE WALINZI

HARARE, ZIMBABWE


SAA chache baada ya Rais wa zamani Robert Mugabe kutangaza kuwa hatampigia kura mrithi na mshirika wake wa zamani, Rais Emmerson Mnangagwa, inadaiwa mkongwe huyo amenyang’anywa walinzi.

Hilo limekuja huku Wazimbabwe wakijitokeza kwa wingi jana kumchagua rais, hasa miongoni mwa wagombea wawili wakuu; Mnangagwa (75) wa chama tawala cha Zanu-PF na kiongozi wa upinzani, Nelson Chamisa (40).

Uchaguzi huo wa rais ulioenda sambamba na ule wa wabunge na madiwani, umesifiwa na waangalizi wa kigeni waliosema mwitikio mkubwa wa wapigakura ulioonekana jana ni fursa nzuri kwa Zimbabwe kuachana na historia mbaya ya nyuma.

Kwa mujibu wa Jealousy Mawarire, ambaye amekuwa msemaji wa Mugabe tangu ang’olewe madarakani Novemba mwaka jana, askari hao tisa waliondolewa saa 11 jioni, ikiwa ni saa tatu tu baada ya Mugabe kumaliza mkutano wake na wanahabari kwenye makazi yake maarufu kama Blue Roof.

“Baada ya Rais Mugabe kuitisha mkutano na wanahabari akisema hatampigia kura Mnangagwa bali mpinzani wake Nelson Chamisa, Serikali iliondoa askari kutoka Blue Roof,” alisema Mawarire ambaye pia ni msemaji wa chama kipya anachohusishwa nacho Mugabe cha National Patriotic Front (NPF).

Alidai kuwa askari hao waliondolewa mara moja baada ya mkutano na kwamba walipora vitu na kufanya uharibifu katika nyumba waliyokuwa wakiitumia.

Hata hivyo, upande wa Serikali haukuweza kupatikana mara moja kuthibitisha au kukanusha madai hayo.

Lakini siku hiyo, Mnangagwa alijibu mapigo dhidi ya matamshi ya Mugabe yaliyolenga kuwavuta wafuasi wake wamuunge mkono pia Chamisa.

Katika kipande cha video kilichosambaa mitandaoni, Mnangagwa alisema: “Sasa iko wazi, ameingia mkataba na Mugabe, hatuwezi kuliamini tena lengo lake la kuibadili Zimbabwe na kulijenga taifa letu.

“Uchaguzi ni wako, umpigie kura Mugabe chini ya kivuli cha Chamisa, au kura kwa ajili ya Zimbabwe mpya chini ya uongozi wangu na Zanu-PF. Mabadiliko ya kweli yanakuja. Tunapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko haya.”

Wakati huo huo, wapigakura jana walimiminika katika vituo vya kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza usiomhusisha kiongozi wa muda mrefu, Mugabe miongoni mwa wagombea.

Kiongozi huyo mwanzilishi wa Zimbabwe huru, alitimuliwa katika mapinduzi mwaka jana baada ya kuwa madarakani kwa takriban miongo minne.

Kura za maoni zinampa uongozi mdogo, Mnangagwa (75), dhidi ya mpinzani wake Chamisa (40) wa Chama cha Movement for Democratic Change (MDC).

Kumeshuhudiwa idadi kubwa ya watu wanaopiga kura kwa mara ya kwanza nchini hapa, huku kura ya vijana ndio inayotazamwa kuwa na uzito kwa vile takriban nusu ya watu waliosajiliwa kupiga kura ni wenye umri wa chini ya miaka 35.

Mamia ya waangalizi wametumwa kuhakikisha uchaguzi unakwenda sambamba, lakini mara kwa mara upinzani umetuhumu kuwapo udanganyifu katika daftari la wapigakura.

Wameelezea wasiwasi pia kuhusu usalama wa makaratasi ya kupiga kura na kunyanyaswa kwa wapigakura hususan katika maeneo ya mashinani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles