22.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Wazee waeleza namna Mwalimu Nyerere alivyojenga Ikulu Chamwino

makerere-at-90-mwalimu-julius-kambarage-nyerere-3Na RAMADHAN HASSAN, CHAMWINO

NI miaka 17 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, atangulie mbele ya haki, ambapo alituachia mambo mbalimbali ya kukumbukwa.

Moja ya mambo ambayo yatakumbukwa ni nia yake ya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi.

Jambo jingine ni kujenga Ikulu katika eneo la Chamwino, mkoani Dodoma, ambapo Rais Dk. John Magufuli ataitumia kutokana na Serikali kuhamia Dodoma.

Nimefunga safari hadi katika vijiji vya Buigiri na Chamwino Ikulu ambapo katika vijiji hivyo Mwalimu Nyerere alijenga Ikulu hiyo kwa kusaidiana na wakazi wa vijiji hivyo.

Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi, anasema kijiji hicho kipo katika Kata ya Buigiri, Tarafa ya Chilonwa, wilayani Chamwino.

Anasema Kijiji cha Chamwino ni cha kihistoria na kiliasisiwa na hayati Mwalimu Nyerere.

Anasema sababu za Mwalimu Nyerere kuchagua Chamwino kuwa Ikulu yake ni pale mwaka 1969 alipotembelea Kambi ya Vijana wa Tanu Youth League, iliyopo katika kijiji hicho.

Yindi anasema alitembelea kambi hiyo Mei 5 mwaka 1969 kuona shughuli za uzalishaji wa zao la zabibu, ukakamavu na utamaduni, katika hotuba yake kambini hapo alitoa agizo kwamba Watanzania wasiishi kama panzi, bali waishi kama nzige.

“Tarehe hiyo hiyo yaani Mei 5, 1969 Mwalimu Nyerere alipanda mlima Matingha ambao siku hizi unajulikana kwa jina la Mongozo, palipojengwa Ikulu ya sasa ya Chamwino ambapo katika eneo hilo kuna nyumba ndogo mlimani ilijengwa kama kumbukumbu yake kwa kupanda mlima huo.

“Alipopanda mlima huo alipendezwa na mandhari aliyoiona ilivyomvutia, aliangalia mteremko wa mlima pande zote, alishauri kambi ya vijana wa Tanu Youth League kuhama kutoka Kitongoji cha Ipala Lya Nhembo kuja kitongoji cha Makungulu Chamwino, ambapo kwa sasa ni kijiji cha Chamwino Ikulu.

“Vijana wa kambi hiyo waliitikia wito, hivyo mwaka 1970 kambi ilihamia mahali alipoainisha Baba wa Taifa na kusema hapo panafaa,” anasema.

Yindi anasema Julai 10 mwaka 1971 ndipo Baba wa Taifa alifika rasmi kuzindua kijiji hicho na alikaa kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Julai 10, 1971 hadi Oktoba 30, 1971 akiishi kwenye hema na kuhakikisha wananchi wanaanza kuhamia.

“Baba wa Taifa pia alishiriki kuchimba mitaro kwa ajili ya usambazaji wa maji kijijini katika vijiji vya Buigiri na Chamwino, lakini kubwa alipenda hali ya hewa ya eneo hilo,” anasema Yindi.

Anasema shughuli nyingine alizofanya katika kijiji hicho ni kusimamia makatapila kufyeka miti maeneo ya mashamba, mbuga ya Madyma ambapo waligawiwa wananchi kulima eneo.

Pia anasema katika eneo hilo kuna Mbuyu uitwao Mwalimu J.K Nyerere, ambao ni kumbukumbu yake na wanakijiji hufanyia mikutano na wanakijiji.

Aidha, anasema alishiriki kufyatua matofali yaliyotumika kujengea Ikulu ndogo iliiyojengwa mwaka 1971, hivi sasa nyumba hiyo inatumika kama nyumba ya wasaidizi wa Rais na huduma mbalimbali za kijamii kwa kutumia mashine iliyotoa matofali 12 kwa wakati mmoja.

Anasema huduma nyingine za kijamii zilizofaidika na matofali hayo ni kujengea ukumbi wa kijiji, ofisi za watendaji wa kijiji, zahanati, shamba la mifugo  ya ng’ombe wa kisasa wa maziwa, ufugaji wa mbuzi wa kisasa, kuku wa kisasa, nguruwe, josho la mifugo, nyumba za watumishi wa serikali ya kijiji.

Pia anasema alishiriki kucheza bao na wazee kwenye mti wa Mnyinga uliopo Kitongoji cha Kambarage baada ya saa za kazi, mti ambao upo mpaka sasa.

Yindi anasema Kijiji cha Chamwino Ikulu kilianza na vitongoji sita vya Kambarage, Mwongozo, Umoja, Maendeleo, Azimio na Ukombozi.

WALIOISHI NAYE WAMZUNGUMZIA

Wakizungumza na gazeti hili, wazee katika Kijiji cha Buigiri wanasema Mwalimu alikuwa na nia ya dhati ya kuwakomboa kiuchumi Watanzania.

Mzee Edward Matewa (94) anasema anachokifanya Rais Magufuli cha kuhakikisha kila mmoja anapata fedha halali ndicho alichokuwa akikifanya Mwalimu Nyerere.

“Alikuwa mtu mwema, alikuja mwaka 1972, nilikaa naye tukazungumza kuhusiana na nia yake ya vijiji vya ujamaa, alitaka watu tuwe pamoja ili tuweze kupata huduma za kijamii pamoja na elimu.

“Ndiyo maana akaja na Azimio la Arusha, nia yake ilikuwa wafanyakazi wasitofautiane sana mshahara, ndicho anachofanya Magufuli kwa sasa,” anasema.

Kwa mujibu wa Mzee Daud Chisandu, ambaye alikuwa kiongozi wa Kitongoji cha Maendeleo enzi za kuanzishwa kwa Kijiji cha Chamwino na hayati Baba wa Taifa mwaka 1971, anasema Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi wa pekee ambaye alikuwa akijituma na kuwapenda watu wake.

“Alikuja hapa Chamwino akakaa na sisi akaanzisha vijiji vya ujamaa, akatufundisha kufanya kazi na kutuhimiza kuhamia kwenye nyumba zilizojengwa kijijini,” anasema.

Naye Lazaro Mchelema, mkazi wa Buigiri,  anasema ukifika katika eneo la Chamwino  Ikulu utaona utofauti na maeneo mengine kutokana na Mwalimu kupanda miti.

Mchelema anasema madhumuni ya Mwalimu kupanda miti kutoka Chamwino Ikulu hadi Buigiri barabara ya Dar es Salaam umbali wa kilomita 3.5 ilikuwa ni kuhifadhi mazingira ili kuleta mandhari nzuri ya Kijiji cha Chamwino na kuhifadhi chanzo kikuu cha maji Chamwino.

Anasema eneo la msitu huo ni zaidi ya hekta 100 kwa eneo linalozunguka kijiji pamoja na miti iliyopandwa pande zote mbili za barabara kutoka Chamwino Ikulu hadi Buigiri barabarani ili kufanya ukanda wa kijani.

“Miti iliyopandwa inastahimili ukame na inayohifadhi maji kama mizambarau, miarobaini, mifuruanji, mitimaji, mijohoro, mipera, miembe, mikaratusi na mikangazi.”

Anasema kutokana na Mwalimu kupanda miti hiyo, kumekuwa ni chanzo kikuu cha maji kwa matumizi ya nyumbani, kunyweshea mifugo na kilimo cha bustani, mbogamboga, nyanya, vitunguu, miwa na matunda.

Mchelema anasema watu wanaokaribia 5,250 wanaotumia maji hayo wanatoka vijiji vya Chamwino, Chinangali, Buigiri na Msanga.

Pia anasema msitu huo wa kupandwa na uoto wa asili imekuwa sehemu ya kutolea mafunzo na utafiti kutoka vyuo  mbalimbali.

Naye Iddi Ngong’ite (80), mwamuzi wa zamani wa mpira wa miguu Tanzania  anasema katu hatamsahau Mwalimu kutokana na nia yake ya kuwasaidia Watanzania.

“Mwalimu jinsi alivyoendesha nchi ndivyo anavyoendesha huyu bwana Magufuli, wanatofautiana kitu kimoja, zamani wezi walikuwa wachache, lakini sasa hivi wamekuwa wengi, hivyo anahitaji nguvu za ziada ili kuweza kufanikiwa,” anasema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamonga, anasema kijiji cha Chamwino Ikulu kinajivunia  shughuli alizofanya Baba wa Taifa, kwani wananchi walifaidika na wanaendelea kufaidika.

Nyamonga anasema wanaendelea kufaidika kwa huduma kama zahanati, upatikanaji wa majisafi na huduma nyingine muhimu.

Anabainisha kuwa, wilaya hiyo inaendelea kuyaenzi mazuri yote yaliyofanywa na Baba wa Taifa kwa kuendelea kuleta maendeleo katika Kijiji cha Chamwino Ikulu, mpaka sasa huduma za msingi zinaendelea kutolewa.

“Japokuwa sina muda mrefu, lakini Mwalimu Nyerere amesaidia sana maendeleo ya Wilaya ya Chamwino,” anasema Nyamonga.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, anasema hayati Baba wa Taifa ameacha historia pana katika Wilaya ya Chamwino kutokana na kupenda watu wake na kumtanguliza Mungu katika mambo yake.

Anasema Mwalimu Nyerere alikuwa na wito kwenye uongozi wake, hali iliyofanya akae kwenye hema ili kuwafikia wananchi na kuwahimiza kwenye shughuli za maendeleo.

“Yeye ndiye aliona umuhimu wa Makao Makuu kuwa Dodoma, hivyo Rais Magufuli amefuata yale ambayo aliyataka Mwalimu, sisi ni kufuata tu,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,057FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles