Beatrice Mosses, Manyara
Wazee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Jimbo la Babati, Usharika wa Babati wamezuia ruzuku ya sadaka zinazopelekwa kwenye dayosisi na majimbo kwa madai kuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk Solomon Masangwa kukataa kumhamisha Mkuu wa Jimbo la Babati, Niiteel Panga.
Sakata hilo lilianza Jumapili iliyopita na jana baada ya Francis Lazaro ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Matengenezo ya Kanisa, kuingilia katikati ya ibada bila ruhusa ya Mchungaji Godlsten Mkenda wa Usharika wa Babati, na kudai wamechoshwa na mienendo ya mkuu huyo wa jimbo.
“Tulikubaliana mama ahamishwe lakini Novemba 2, mama akarudi Jimboni tukasema sawa tumuache akae kae ofisini, Novemba 6 tulikaa tukafanya kikao chetu cha tathmini kuwa mama amesharudi sasa tunafanyaje, tukakubaliana kwamba kwa kuwa amerudi na sisi hatuna haja ya kupigana nae cha msingi hapa ni kuanza kuzuia sadaka.
“Mmemsikia mzee wa Kanisa alivyosema kwenye matangazo kuwa taarifa nyingine mtasikia baadae ni kwamba hakuna uwiano ulioenda usharikani, jimboni wala Dayosisi, sadaka zote za Jumapili iliyopita zipo kwenye akaunti ya mtaa kwa hiyo niwaombe sana leo tutoe sadaka kwa wingi maana zinaingia kwenye akaunti ya mtaa iliyopo Benki ya Posta na fedha zenu ziko salama kabisa,” amesema.
Pamoja na mambo mengine amesema Novemba 13 walikaa kikao wakakubaliana lazima kuwe na maazimio na azimio la kwanza ni lazima mkuu wa jimbo ahamishwe, azimio jingine ni kuendelea kuchukua sadaka zote na kupeleka kwenye akaunti ya mtaa.
“Azimio kama Dayosisi haitamuhamisha mkuu wa jimbo tutapeleka kesi mahakamani na tutamfungulia kesi ya udhalilishaji na tunazo ‘clip’ nne zilizosimama,” amesema Lazaro.