Na Allan Vicent, Tabora
Umoja wa Wazee Wastaafu wilayani Nzega Mkoani Tabora (UWANZE) wameukaribisha mwaka mpya 2021 kwa kufanya harambee ya kutunisha mfuko wa  kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Katika harambee hiyo jumla ya Sh 700,000 zilikusanywa papo hapo kwa ajili ya mfuko huo ili kuanza mchakato wa kuanzisha miradi yao.
Wakizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika juzi katika ukumbi wa Lake Tanganyika wilayani hapa walisema kuwa wanataka mwaka 2021 kuwa mwaka wa tofauti katika maisha yao.
Walibainisha kuwa awali walikuwa na miradi ya kilimo lakini haikuwasaidia chochote kutokana na kukosa usimamizi mzuri na hali ya hewa kutoeleweka.
Mwenyekiti wa Umoja huo Aron Maganga alieleza kuwa mwaka 2017 walitenga ekari 6 kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha alizeti lakini hakikufanikiwa kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya.
Alibainisha kuwa mwaka huu 2021 wamepanga kuanzisha biashara ya kuuza sukari, saruji na ufugaji kuku wa kienyeji ili kujikwamua kiuchumi.
Mgeni rasmi katika harambee hiyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wilayani hapa, Issa Mwinyimvua, aliwapongeza wazee hao kwa kuchukua umaskini na kufikiria kuanzisha miradi ya kimaendeleo ili kujiongezea kipato.
Aliwashauri kutumia taasisi za kifedha ili ziwawezeshe mikopo yenye riba nafuu na ushauri wa kibiashara huku akisisitiza uaminifu na usimamizi mzuri wa fedha zao ili kuwa na miradi endelevu na yenye ufanisi.
Aidha aliwataka kuhamasishana ili wazee wengi zaidi wajiunge na umoja huo na kuanzisha miradi ya pamoja itakayokuwa endelevu ili kujikwamua kiuchumi.
Naye diwani wa kata ya Nzega Mashariki, Salim Haruna aliahidi kushirikiana na wazee hao na kuwataka kuendelea kuonya au kukemea viongozi na watendaji wa serikali wanaoenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.