26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi,walezi waaswa kuzingatia malezi

Faraja Masinde -Dar es salaam

WAZAZI na walezi, wameaswa kuzingatia suala la malezi kwa watoto ngazi ya familia kwa sababu bado ni changamoto na limekuwa likileta matatizo mbalimbali.

Miongoni mwa matatizo hayo, ni kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi wao na wengi kukimbilia kuishi mitaani.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, wakati wa kongamano la kitaifa la waandishi wa habari juu ya agenda ya kitaifa kuhusu wajibu wa wazazi na walezi katika malezi na matunzo ya familia liliwakutanisha wahariri na waandishi wa habari zinazohusu watoto, malezi na matunzo ya familia.

Akizungumza kwa niaba ya, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Mwajuma Magwiza alisema utafiti  uliofanywa na wizara kwa kushirikiana na wadau Desemba, mwaka juzi hadi Januari, mwaka jana katika halmashauri za Ilala, Kinondoni, Temeke, Kigamboni, Ubungo, Arusha, Iringa, Mbeya Jiji, Wilaya ya Mbeya, Dodoma, Nyamagana na Ilemela iligundua uwapo watoto 6,393, ikiwa watoto wa kike 1,528 na watoto wa kiume  4,865 wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Alisema kati yao watoto 1,385 watoto wa kike  410 na watoto wa kiume 975, walitambuliwa wakiishi na kufanya kazi mitaani muda wa usiku uwepo wa watoto hawa maeneo ya mitaani kwa kiasi kikubwa unatokana  na kutowajibika kwa familia katika kumudu majukumu yao ya kutunza na kulea watoto wao.

Alisema kulingana na taarifa ya utafiti wa afya ya mama na mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2015/16, inaonesha asilimia 25 ya kaya za mijini na asilimia 27 ya kaya za vijijini zina watoto ambao hawaishi na wazazi wao japokuwa mzazi mmoja au wote wawili bado wapo hai, hii inamaana wanaishi katika familia pana au wao wenyewe peke yao hivyo kukosa malezi ya wazazi wa pande zote mbili yaani baba na mama katika makuzi yao.

“Hii inawaathiri watoto kisaikolojia, wakati mwengine inasababisha na kuchangia kwa kiasi kikubwa watoto kuamua kuondoka na kwenda maeneo mengine ikiwemo mitaani, kujishughulisha na shughuli hatarishi kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao,” alisema Mwajuma.

Alisema kwa kuthamini na kutambua umuhimu wa familia katika malezi na matunzo, Serikali imendaa ajenda  ya kitaifa ambayo inalenga  kuhakikisha wazazi na walezi na jamii kwa ujumla inakumbushwa na kuhimizwa kuwajibika kuwapa matunzo na malezi bora watoto.

“Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutenga muda wa kuwa na vipindi mahsusi vya kuwakumbusha na kuwaelimisha wazazi na walezi wajibu wao kuwalea, kuwatunza, kuzungumza na kuwapa upendo watoto ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanakuwa salama na kufikia ndoto zao na  kuwa wazazi bora wa baadae,” alisema Mwajuma.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mkurugezi Msaidizi sehemu ya Familia kutoka Wizara ya Afya, Tausi Mwilima alisema ili kuhakikisha familia inasimama imara na kutimiza wajibu wake katika kutoa malezi chanya wizara imeandaa ajenda hiyo ya kitaifa ambayo inaweka msisitizo katika maeneo makuu matano.

Alisema katika kongamano hilo, watatoka na mpango kazi wa pamoja wa namna bora ya kutekeleza ajenda hii kupitia vipindi mbalimbali.

“Wizara imejipanga kuhakikisha  elimu hii inawafikia wadau mbalimbali makundi maalumu ya kimkakati, tumeanza na kundi la wanahabari watakaoshirikiana na Serikali  kuhakikisha ajenda hii inatekelezwa na kila mtu, vikiwamo vyombo vya habari,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles