Na HARRIETH MANDARI
POLISI Mkoa wa Geita wanawashikilia wazazi wa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Wezela mwenye umri wa miaka 12 kwa kumkatisha masomo binti yao na kumuozesha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo aliwataja wazazi hao kuwa ni Costantine Elias na Lugazia Kobekobe wakazi Kijiji cha Wezela Tarafa ya Bugando.
Alisema wazazi hao kwa sasa wanashikiliwa na polisi na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Mwabulambo alisema kuozeshwa kwa mwanafunzi huyo kulibainika baada ya mahudhurio yake kuwa hafifu shuleni.
Alisema jambo hilop lilitia shaka kwa walimu na katika kufuatilia walielezwa na wasamaria wema kuwa alikuwa ameozeshwa na wazazi wake na kwa mwanamume wa miaka 18.
“Walileta taarifa kwetu na kuanza ufuatiliaji, kutokana na ushirikiano wa wanafunzi wenzake na waalimu, tulifanikiwa kumkuta nyumbani kwa Sadick Costantine (18) ambaye alidaiwa kuwa ndiyo mumewe na sasa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi,”alisema.
Kaamanda Mponjoli alisema uchunguzi ulibaini binti huyo ambaye alikuwa anaishi na mlezi wake, Lugazia Kobekobe, aliozwa kwa idhini ya mzazi wake, Costantine Elias na mama yake, Leah Msendamila, kwa mahari ya ng’ombe mmoja na mbuzi mmoja.
“Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, mtu yeyote atakayeshiriki kushawishi au kutoa idhini kwa binti chini ya miaka 18 kuolewa anakuwa amevunja sheria,”alisema.
Kamanda Mponjoli alisema kwa mujibu wa kifungu ha sheria namba 13:1 ni makosa kwa mtu kuoa binti chini ya miaka 18 bila kupata ridhaa kutoka mahakamani.
Alisema katika maeneno mengi mkoani humo yamekuwapo matukio mengi kama hayo lakini takwimu sahihi zinakuwa ngumu kupatikana kutokana na kukosekana ushirikiano kutoka kwa jamii ambao wengi hufanya kwa siri.
“Matukio ya aina hii yapo katika maeneo ya Mkoa wa Geita kutokana na mila na desturi ambako binti mdogo anaweza kuozwa au kijana mdogo kuoa hata kama ni mwanafunzi,” alisema.