32.2 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

Wazazi Kusini Unguja wafundwa ujasiriamali kujikwamua kiuchumi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Viongozi 60 wa Jumuiya ya Wazazi kutoka Wilaya ya Kusini Unguja Zanzibar wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo hayo ambayo yamehusisha utengenezaji sabuni za maji, dawa za kuua wadudu na mkaa mbadala yalitolewa kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Wazazi Ilala huku wawezeshaji wakiwa ni Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Kimanga, Niwendo Juma (Katikati), akishirikiana na viongozi wengine kutengeneza mkaa mbadala baada ya kupatiwa mafunzo na Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kata ya Kimanga, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Ilala, Mohamed Msofe, amesema yanalenga kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Mafunzo haya yatadumisha undugu baina yetu Ilala na wenzetu wa Kusini unguja na kujikwamua kiuchumi, tunataka mtu asiwe mwanasiasa tu halafu hana kitu cha kufanya ndiyo maana tunapeana ujuzi wa kujikwamua kiuchumi,” amesema Msofe.

Amesema pia jumuiya hizo zimejiwekea utaratibu wa kuwezeshana kiuchumi na kwamba Julai mwakani Ilala nao watakwenda Zanzibar kujifunza masuala mbalimbali.

Naye Katibu wa Wazazi Wilaya ya Kusini Unguja, Fadhili Wima, amesema watayatumia vizuri mafunzo hayo ili iwe chachu ya kujikwamua kimaisha.

“Tumefarijika sana kupata mafunzo haya, lengo la safari limekamilika kwa sababu wengine tulikuwa hatuna taaluma hiyo, tumekuja wachache na Wilaya ya Kusini tuna wanachama wengi hivyo, tutakwenda kutoa elimu hii kwa wanachama wengine na wasio wanachama ili waweze kupata ujuzi huu,” amesema Wima.

Mshiriki mwingine ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa Wadi ya Makunduchi iliyopo Wilaya ya Kusini, Fatuma Badru Mwita, amesema atakaporudi Zanzibar atakuwa mwalimu wa kuwafundisha wengine yale waliyojifunza.

“Tumetengeneza sabuni za maji, dawa za kuondoa madoa, dawa za kuua wadudu na mkaa mbadala, nashukuru si haba nimejifunza,” amesema Mwita.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Kimanga ambao ndio wenyeji, Niwendo Juma, amesema wataunda vikundi vya ujasiriamali kwa kila tawi ili kusambaza mafunzo hayo kwa wanachama wengine.

“Nina matawi sita na mitaa mitano kwahiyo tutakaa kamati ya utekelezaji ya kata kisha tutatembelea matawi yote kupeleka mafunzo haya,” amesema.

Mwezeshaji katika mafunzo hayo Mkurugenzi wa Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, amewataka washiriki hao kuwa wabunifu na kutengeneza bidhaa kulingana na mahitaji ya soko.

Viongozi hao pia wamepatiwa semina ya uongozi pamoja na kutembelea Chuo cha Ufundi cha Wazazi kilichopo Buguruni na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Dar es Salaam mpaka Pugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles