27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi Ilala wajielekeza kufanya siasa na uchumi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala katika ngazi ya matawi na kata wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha kufanya shughuli za kujiingizia kipato badala ya kutegemea siasa pekee.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Baraza Kuu la Wazazi Taifa, Seleman Juma Kimea (aliyevaa kofia), akiwa na viongozi wengine wa jumuiya hiyo wakipata mafunzo ya utengenezaji sabuni.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na jumuiya hiyo na kufanyika katika Kata ya Kipunguni yanahusisha utengenezaji keki, mkaa mbadala, sabuni, urembo mbalimbali kwa kutumia shanga pamoja na ufugaji.

Akifungua mafunzo hayo Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa Jumuiya ya Wazazi, Sudi Kassim, amesema jumuiya hiyo haitaki kutegemea siasa tu ndiyo maana wanaendesha mafunzo ya ujasiriamali ili watu waweze kupata kipato cha ziada kuendesha maisha yao.

“Chama kimejielekeza kufanya siasa na uchumi ndiyo maana kuna programu mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali kwa wanachama ili baada ya kufanya siasa mtu awe na kipato cha kuendesha maisha yake,” amesema Kassim.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala, Mohamed Msofe, amesema mafunzo hayo yana lengo la kuamsha jumuiya hiyo ili wanachama waweze kujifunza mambo mbalimbali yatakayowanyanyua wao na wananchi wote kwa ujumla.

“Tumegundua watu wengi wanachukua mikopo ya manispaa lakini wanakuwa bado hawajajipanga nini wafanye, tukiwapa mafunzo ya vitendo mtu ataelewa anachukua mkopo anakwenda kuufanyia nini,” amesema Msofe.

Mwezeshaji katika mafunzo hayo Selemani Bishagazi ambaye ni Mkurugenzi wa Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, amesema washiriki pia wamefundishwa namna ya kuandika wosia na kufahamu sheria kandamizi zinazomkandamiza mwanamke na namna mwanajamii anavyoweza kushiriki kuondoa ukatili.

“Mwanajamii akijifunza kutengeneza mkaa kwa kutumia takataka zinazomzunguka ataweza kuokoa Sh 2,000 ambayo ataitumia kwa matumizi mengine,” amesema Bishagazi.

Mkurugenzi wa Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi, akiwaeleza viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala kuhusu ufugaji kuku aina ya Kuchi ili waweze kujiongezea kipato.

Mafunzo hayo pia yalishirikisha baadhi ya wanachama wa jumuiya hiyo kutoka Zanzibar ambapo Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Baraza Kuu la Wazazi Taifa, Seleman Juma Kimea, aliwataka washiriki kutumia elimu waliyoipata kwa kwenda kuwafundisha wengine.

Mmoja wa washiriki Raya Nyange Ali ambaye ni Ofisa Tehama Jimbo la Chahani Zanzibar, amesema atatumia vema fursa ya mafunzo hayo aweze kutatua changamoto zinazomkabili yeye na vijana wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles