29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi asilimia 70 wanakwepa majukumu ya familia za

Na BENJAMIN MASESE-SIMIYU

MWENYEKITI Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dk. Titus Kamani amesema asilimia 70 ya Watanzania wenye familia zao hawawajibiki ipasavyo katika kutimiza wajibu wao.

Alisema hatua hiyo imesababisha Serikali  na wanasiasa kuwa na mzigo mkubwa wa kuelimisha jamii namna ya kuishi na kupata maendeleo.

Kauli hiyo aliitoa juzi katika Kijiji cha Mkula Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wakati wa uzinduzi wa kitabu cha historia ya maisha ya  Mzee Lufulondama Nteminyanda (84) ambaye anatajwa kuwa aliishi kwa umasikini mkubwa huku akiwasomesha watoto na kutengeneza familia bora na mfano kwa Watanzania wengine.

Mzee Nteminyanda ambaye ana watoto 33, wajukuu 81 na vitukuu 18 alioa wanawake watatu wawili wakiwa ni wa familia moja na kuishi nao kwa upendo.

Dk. Kamani ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema 

kuwa asilimia 70 ya wazazi  nchini hawatimizi wajibu wao ndani ya familia badala yake wanaiachia serikali na jamii kutoa elimu, maadili, utamaduni ,ushauri na maelekezo ya namna ya kufanya shughuli za maendeleo ili  kujikwamua kiuchumi.

“Baadhi ya wazazi  hasa wanaume tumebaki kuwapa  tu  ujauzito wake zetu na kuwaacha  bila matunzo na malezo bora, mtoto anakuwa ndani ya familia hana maadili, anapelekwa shule na kuwaachia walimu  bila kushirikiana kumlea isitoshe baadhi ya familia dada wa kazi ndiye anaachiwa majukumu yote ya kuwatunza watoto, hii ni hatari sana.

“Mfano Mzee Nteminyanda ambaye akiwa kijana aliweza kuishi kwa ndugu baada ya wazazi wake kufariki lakini alipofikisha umri wa miaka 22 aliweza kujitegemea na kujihusisha na kilimo, ufugaji, biashara ya pilipili na ngozi.

“Aliweza kuoa mke wa kwanza na kuishi naye kwa kufanya kazi jambo ambalo lilimfanya baba mkwe kumpatia binti mwingine kama mke wa pili, leo tunaona matunda yao.

“Hapa mnawaona viongozi mbalimbali wa Serikali wamekuja kushiriki tukio hili la uzinduzi wa kitabu cha Mzee Nteminyanda, hawajaja kwa bahati mbaya bali watoto wake mzee huyu nao ni watumishi wa serikali tena wakubwa  na wengine ni mabosi wetu.

 “Kikubwa tunawaomba Watanzania wawajibike katika familia zao, yapo mambo yanayotakiwa kufanywa na Serikali kwa watu wake lakini hivi sasa viongozi wa Serikali wanawajibika kufanya mambo ndani ya jamii ambayo yalitakiwa kutimizwa na wazazi.

Kwa upande wake, Mzee Nteminyanda aliitaka jamii na kubadili mfumo wa maisha, mitazamo na uelewa katika kufanya kazi nje ya mazoea au kutenda jambo kulingana na mazingira.

Alisema vijana wamejengwa katika fikra za kuajiriwa jambo ambalo limetengeneza kundi kubwa lenye fikra ya kusubiri ajira bila kujali umri wao licha ya Serikali kutokuwa na uwezo.

“Ongezeko la vijana wasiokuwa na ajira ni kubwa sana na linatishia taifa na jamii  kwani katika siku za usoni kutakuwa na kundi la vijana  tegemezi wengi na madhara ya utegemezi kwa vijana watakapokuwa wazee wataigharimu Serikali kwa kuhitaji  iwatunze.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles