WAZANZIBARI wanaoishi nchini Uingereza jana wamefanya maandamano kutaka nchi hiyo iingilie kati na kutoa shindikizo kwa Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar anatangazwa na kuapishwa.
Hatua ya maandamano hayo yamekuja kutokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo huku akitoa sababu tisa ikiwemo uchaguzi kutoka huru na haki.
Katika maandamano hayo hayo yaliyofanyika nchini humo na kukusanya sehemu ya Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza, walifanya maandamano hayo ambayo yaliishia katika Mtaa wa Downing zilipo ofisi za Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na kukabidhi barua yao.
“Tumefanya maandamano ambayo yameratibiwa na viongozi wa Zanzibar Welfare Association (ZAWA) na tumefikisha ujumbe wetu, ambapo tumekwenda hadi katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron katika namba 10 Downing Street na kukabidhi barua yatu,” alisema mmoja wa viongozi wa ZAWA
Tangu kufutwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi mataifa kadhaa ya nje yamekuwa yakiingilia hatua hiyo ikiwemo Serikali ya Marekani na kutaka tamko hilo liondolewe.
Serikali ya Marekani imesema imeshtushwa sana na tamko la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.
Katika tamko lililotolewa na ubalozi wa Marekani nchini, umesema hatua hii inasitisha mchakato wa uchaguzi uliofanyika vizuri na kwa amani, kama ilivyoelezwa na waangalizi wa uchaguzi kutoka Ubalozi wa Marekani, Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na kusitisha zoezi la majumuisho ya kura lililokuwa linakaribia kukamilika.
“Tunatoa wito wa kuondolewa kwa tamko hilo na kuzisihi pande zote kudhamiria kwa dhati kuukamilisha mchakato huu wa kidemokrasia kwa uwazi na kwa amani. Watu wa Zanzibar wanastahili jambo hilo,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na ubalozi wa Marekani nchini kwa vyombo vya habari.
Awali Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, alisema kuwa wameamua kufuta uchaguzi huo baada ya kubaini kasoro tisa, ikiwamo kuchezewa kwa matokeo katika Kisiwa cha Pemba.