FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Ilala inawashikilia watumishi wawili wa Manispaa ya Ilala kwa kosa la ubadhilifu wa zaidi ya Sh milioni 100 za ujenzi wa Zahanati.
Watumishi hao ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kipunguni, Joven Challange na Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Machimbo, Deogratius Tesha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Takukuru Ilala, Christopher Myava amesema fedha hizo zilizokuwa za ujenzi wa ofisi ya kata zilibadilishwa matumizi na kuelekezwa katika ujenzi wa Zahanati.
Amesema kwa nyakati tofauti watuhumiwa waliokuwa watia saini katika akaunti hiyo iliyopo benki ya Dar es Salaam Community Bank (DCB) walitoa fedha kwa manufaa yao binafsi.
“Watuhumiwa ambao ni watia saini wa akaunti hiyo walikuwa wakitoa fedha hizo za miradi ya maendeleo kwa manufaa yao binafsi,” amesema Myava.