31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAWEKEZAJI WA MADINI WAPEWA MAELEKEZO

Na ABRAHAM GWANDU–ARUSHA          |         


TUME ya Taifa ya Madini imewaagiza wawekezaji katika sekta hiyo nchini, kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo.

Katika ushiriki huo, tume hiyo imewataka wawekezaji hao kurejesha kiasi cha faida wanayopata kwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Agizo hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Idris Kikula, alipokuwa akizungumza wakati wa ziara ya tume yake katika machimbo ya migodi ya vito aina ya rubi yanayochimbwa wilayani Longido, Mkoa wa Arusha.

Katika maelezo yake, Profesa Kikula alisema kuanzia sasa migodi yote inatakiwa ijielekeze katika uwekezaji unaojali masilahi ya wananchi hasa wale wanaozunguka maeneo wanayofanyia kazi.

“Ni jambo lisiloeleweka kukuta maeneo yanakochimbwa madini yenye thamani, wananchi wa maeneo hayo hawana maji safi na salama kwa matumizi yao na pia hakuna zahanati au shule kwa ajili ya watoto kupata elimu.

“Serikali ina majukumu mengi na makubwa ya kutekeleza kwa manufaa ya Taifa, kwa hiyo ni wajibu wenu wawekezaji kuona ni kwa namna gani na nyinyi mtasaidia katika kuiunga mkono Serikali hasa kwenye sekta ya elimu, maji, afya pamoja na huduma nyingine muhimu.

Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma, alisifu uwekezaji na uchimbaji unaofanywa na Kampuni ya Mundarara Mining Longido kwa kile alichosema ni wa kisasa na hauwezi kusababisha ajali.

“Tumezunguka na kujionea hali ilivyo katika migodi ya wawekezaji wazawa na hapa nyie Mundarara mnahitaji kupongezwa kwa sababu uchimbaji wenu ni wa kisasa.

“Hata wafanyakazi wote ajira zao ni za hakika na hazina utata kwenye mikataba yao, vifaa vya uchimbaji, vifaa vya utoaji na uvutaji hewa chafu ni vya kisasa kabisa.

“Tumeona wafanyakazi wana ari ya kazi, hii ni nzuri sana kwa mwekezaji wa ndani wa madini na tunataka wawekezaji wengine waige mfano wa kampuni hii,” alisema Profesa Mruma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles