23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wavuvi Mafia wataka warudishiwe wake zao

GUSTAPHU HAULE-PWANI

ZAIDI ya wavuvi 430 waliopo katika Kisiwa cha Nyororo Wilayani Mafia wamemuangukia  Rais Dk.John Magufuli ili awasaidie kutatua kero zao ikiwemo ya kurudishiwa wanawake zao waliondolewe katika kisiwa hicho kwa amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaibu Nunduma bila kutoa sababu.

Mbali na hilo lakini pia kero nyingine ni pamoja na kupangiwa muda na idadi ya wavuvi wanaotakiwa kuishi katika kisiwa hicho jambo ambalo limekuwa likiathiri vijana na wavuvi kiujumla kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji kwa kujiamini.

Mapema wiki iliyopita Mkuu wa Wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Shaibu Nunduma alitoa kauli ya kuamuru wanawake wote waliopo katika kisiwa hicho kuondoka mara moja ili kibaki na wanaume pekee huku pia akitaka watakaoishi wawe ni wavuvi 100 kwa awamu tofauti.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu uliofanyika kusiwani hapo juzi baadhi ya wavuvi hao walisema kuwa kitendo cha kuwaondoa wanawake katika Kisiwa hicho ni kuleta ubaguzi ambao kwa nchi ya Tanzania bado haijafika huko.

Joseph Mwang’onde,ambaye ni kiongozi wa dini na mvuvi wa kisiwani humo alisema kuwa wao wapo kisiwani humo tangu mwaka 2016 na wanaendesha maisha yao pamoja kuhudumia familia zao kupitia shughuli za uvuvi wanazozifanya kisiwani humo.

Alisema kuwa  kila mvuvi aliyekuwepo kisiwani humo amekata kibali ( leseni) maalum ya kuhalarisha uvuvi wake lakini wanashangaa kuona mkuu wa wilaya hiyo anatoa amri ya kutaka wavuvi waondoke na hata kuwafukuza wanawake zao bila sababu za msingi.

Naye Hamisi Mohamed, alisema kuwa anashangaa kuona mkuu wa Wilaya hiyo anakuwa kigeugeu kwani awali alipokwenda kisiwani humo aliwakutana wanaishi wanaume pekee yao zaidi ya 600 na kusema haiwezekani waishi bila wanawake hivyo wafanye jitihada za kuwaleta wanawake.

Alisema alisema kuwa baada ya kufanya jitihada za kuwapeleka wanawake katika kisiwa hicho mkuu huyo wa wilaya amewageuka na kuanza kuwafukuza wanawake wote na kwamba kwasasa wanaishi wanaume pekee zaidi ya 430 bila wanawake.

“Sisi tunashangaa kuona mkuu wa wilaya anawafukuza wanawake kisiwani humu ili tuishi wanaume pekee, Sasa tunauliza anataka kuhalarisha ndoa ya jinsia moja? na je ,ni maeneo gani ya Tanzania yamehalarishwa wanaume waishi pekee yao mbona visiwa vingine wanaishi wanaume na wanawake kwanini hapa Nyororo wanawake wanafukuzwa? ,” alihoji Mohamed.

Rehema Seif, mmoja wa wanawake mjasiriamali kutoka Tandale Dar es Salaam  alisema kuwa alifika kisiwani humo baada ya kusikia Kuna wavuvi wanaishi pekee yao na kuanza kujenga banda la biashara.

Alisema kuwa yeye alifika hapo kufanya biashara lakini mtaji wake alikopa na alitarajia kurudisha baada ya kufanya biashara lakini baada ya miezi mitatu alishangaa mkuu wa wilaya anawafukuza.

Alisema kuwa, baada ya kusikia amri ya mkuu huyo waliandika barua na kwenda ofisini kwake lakini hatahivyo aliwaamuru waondoke na kusema ifikapo Jumapili ya Februari 16, mwaka huu angepeleka wanajeshi kuwaondoa.

“Sisi tunaomba haki itendeke,hivi ni eneo gani la Tanzania wanaishi wanaume bila wanawake ? tumekuja kufanyabiashara ili tupate kipato,tunaomba Rais Magufuli aliangalie jambo hili,” alisema Rehema.

Kwa upande wake katibu wa kisiwa hicho,  Omary Mohamed, alisema kikubwa anachokishangaa ni kuondolewa kwa wavuvi katika kisiwa hicho kwani tangu mwaka 2016 kisiwa hicho kimekuwa na watu 600 mpaka 700.

Alisema kuwa watu wote waliokuwepo wakiishi katika kisiwa hicho wamekata leseni halali na wanalipa kodi kama kawaida na kwamba sasa wamelipa kodi kiasi cha Sh milioni 103 ambazo zimepokelewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia.

Alisema kuwa,mwaka 2016 walikusanya mapato ya Sh milioni 28, mwaka 2017 walikusanya milioni 24,2018 walikusanya  milioni 25 wakati 2019 walikusanya milioni 24 ambapo kushuka kwa mapato hayo kunatokana na baadhi ya wavuvi kuondoka kwa amri ya mkuu huyo wa wilaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles