26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Wavamizi chanzo cha mto Sola kushughulikiwa-DC Maswa

Na Samwel Mwanga, Maswa

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge ameagiza kuchukuliwa hatua za haraka kuwadhibiti watu wote waliovamia eneo la mto Sola ndani ya mita 60 na kufanya shughuli za kilimo kinyume cha sheria.

Mkuu hiyo wa wilaya ameagiza kupatiwa majina ya watu wote waliovamia eneo la bonde la mto huo ambao umekuwa ukitiririsha maji yake katika bwawa la New Sola(Maarufu Bwawa la Zanzui) ambalo ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji wa Maswa na vijiji 12.

Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Aswege Kaminyoge(aliyepo mbele mwenye kofia)akizungumza na watumishi wa serikali na viongozi wa wilaya hiyo walioshiriki zoezi la upandaji miti kwenye hifadhi ya Mto Sola.(Picha Na Samwel Mwanga)

Hatua hiyo imekuja wakati wa zoezi la upandaji miti katika eneo la bonde la Mto Sola ambapo Kaminyoge amejionea watu wakiwa wamelima mashamba ndani ya mita 60 ndani ya eneo la mto huo licha ya kuzuiwa kufanya shughuli zozote za kibinadamu zikiwemo za kilimo,ujenzi na ufugaji.

“Tulifanya kikao na wananchi wenye maeneo kandokando ya mto Sola tukakubaliana ya kuwa hakuna kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya Mita 60 na tukapima lakini baadhi yao wamekiuka sheria na wamelima hilo jambo halikubaliki ni lazima tuchukue hatua.

“Mto huu wa Sola ni muhimu sana ndiyo unaotiririsha maji yake kwenye bwawa la New Sola ambalo ndicho chanzo kikuu cha maji kwa mji wetu wa Maswa na vijiji 12 hivyo ni lazima chanzo hiki tukilinde kwa nguvu zote,” alisema.

Pia amezitaka idara zote zinazohusika na masuala ya utunzaji wa Mazingira zikiwemo Wakala wa Misitu Nchini(TFS), Idara ya Mazingira na Afisa Misitu kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kikamilifu kwa kutunza mazingira yakiwemo ya vyanzo vya maji kikiwemo chanzo hicho.

Alisema ni vizuri kwa halmashauri ya wilaya hiyo kulipa kipaumbele suala la mazingira kama ilivyo kwa masuala ya Ukimwi na Lishe.

Zoezi la upandaji miti katika bonde la mto Sola katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kwa lengo la kuhifadhi mazingira katika mto huo

“Halmashauri lifanyeni suala la mazingira kuwa agenda ya kudumu katika vikao vyenu kama ilivyo kwa Ukimwi na Lishe maana mazingira yakiharibiwa ndiyo maana kuna kuwa na mabadiliko ya tabia nchi na kusababisha mvua kutonyesha na vyanzo vya maji kutoweka na huvyo kuathiri maisha ya viumbe hai tukiwemo sisi binadamu,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Mary Misangu alisema kuwa wakuu wengi wa idara katika halmashauri hiyo wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ya kuwasimamia wananchi ndiyo maana vyanzo vya maji vinaingiliwa na kufanyika shughuli za kibinadamu huku wakiangalia bila kuchukua hatua.

Alisema kuwa kitendo cha Afisa Mazingira wa wilaya hiyo kushindwa kuzuia watu kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya ndani ya mto Sola ni lazima wachukue hatua dhidi yake kwa kushinda kutekeleza majukumu yake.

“Ni lazima huyu Mkuu wa kitengo cha Mazingira atueleze kwa nini ameruhusu watu kulima kwenye eneo la mto Sola huku akishindwa kuchukua hatua kwa watu waliokiuka sheria ya mazingira hatuwezi kuwa na wataalam ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(Mauwasa),Mhandisi Nandi Mathias alisema kuwa Mto Sola unachangia kuingiza maji katika bwawa la New Sola kwa asilimia 75 hivyo ni vizuri chanzo hicho kikalindwa kwa gharama zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles