27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

WAUZAJI DAWA ZA KULEVYA WAWAFUATA MATEJA VITUONI

VERONICA ROMWALD NA KAMILI MMBANDO – DAR ES SALAAM


WAUZAJI wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya kwa kuwafuata na kuwashawishi waathirika wa dawa hizo wasitumie tiba yoyote vinginevyo watakufa.

Kutokana na watumiaji wa dawa za kulevya kukimbilia katika vituo vya tiba na nyumba za ushauri nasaha wauzaji wameamua kuwafuata moja kwa moja katika vituo hivyo ambako mateja wengi wamejisalimisha.

Akizungumza na MTANZANIA jana, mmoja wa waathirika wa heroin ambaye kwa sasa anapata tiba ya methadone katika Hospitali ya Mwananyamala, Kubushe Ngoi alisema ameshuhudia wauzaji kila siku wakiwafuata hospitalini hapo.

“Binafsi nina muda mrefu kidogo tangu nianze kupata tiba ya methadone kabla ya serikali kuanzisha vita hii sikuwahi kuwaona watu wakija eneo hili kutushawishi kuacha matibabu.

“Unakuta mtu umewahi hospitalini na kupanga foleni upate namba ya kumwona daktari, mtu yupo nje ya geti anakuita ukazungumze naye, ukienda anaanza kukushawishi kuachana na methadone kwamba eti zinasababisha mtu kufa haraka,” alisema.

Inaelezwa kuwa hivi sasa dawa za kulevya zimeadimika mitaani na wafanyabiashara  wachache walionazo wanaziuza kwa bei kubwa na kuwafanya wateja wao kushindwa kumudu gharama hizo.

Kutokana na kuadimika huko idadi ya waathirika wa dawa hizo wanaofika katika hospitali mbalimbali zinazotoa dawa ya methadone nayo imeongezeka maradufu.

Jana Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangala amelitaka Jeshi la Polisi kuweka ulinzi katika vituo vya tiba ili kudhibiti watu wanaokwenda kuwashawishi waathirika kuacha kutumia methadone.

Akiwa Hospitali ya Mwananyamala jana, Dk Kigwangala alisema wamegundua mbinu hiyo inayowafanywa na wauzaji na kwamba wamejipanga kikamilifu kupambana nao kwa namna yoyote ile ili kuokoa Taifa.

“Tunatambua vita hii si ndogo na si ya mtu mmoja, ni ya Watanzania wote. Wakati Kamishna Sianga akipambana na udhibiti, Wizara ya Afya sisi tutatoa tiba kwa waathirika maana tunawahitaji kwani ni nguvu kazi ya Taifa,” alisema.

Vita ya dawa za kulevya imeanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mapema mwezi huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles