23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Wauguzi na wakunga watakiwa kuzingatia kanuni, maadili

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Dodoma

Wauguzi na wakunga nchini wametakiwa kutekeleza misingi saba ya kanuni na maadili ya taaluma hiyo ili kutoa huduma bora na zenye staha.

Wito huo umetolewa Agosti 4,2024 na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Agnes Mtawa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Agnes Mtawa, akizungumza na waandishi wa habari
kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

TNMC inashiriki Maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali kama vile uhuishaji wa leseni, usajili na utoaji wa elimu ya sheria na maadili kwa wauguzi na wakunga na kutoa elimu ya haki ya mteja akiwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Ameitaja misingi hiyo kuwa ni kuheshimu utu, mila na desturi na kwamba wanapomhudumia magonjwa wamhudumie bila kumlinganisha na mtu mwingine.

Ofisa Uhusiano wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Ezekiel Nyalusi, akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea banda la baraza hilo kwenye Maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

“Ni lazima muuguzi, mkunga apate idhini ya mteja kabla ya kutoa huduma, mgonjwa aelezwe anapata huduma gani na muuguzi ahakikishe anawajibika na kile anachokifanya, kama anampa dawa ahakikishe anafuata taratibu ili chochote kinachotokea awajibike mtoa huduma na si mtu mwingine,” amesema Mtawa.

Amesema pia ni lazima muuguzi, mkunga afanye kazi kama timu ili magonjwa aweze kutibiwa na timu husika na kutunza siri za magonjwa.

Kulingana na msajili huyo, muuguzi, mkunga anapaswa kujiendeleza kitaaluma kwa sababu masuala ya afya yanabadilika kila siku.

“Muuguzi, mkunga anapaswa kuwa mwaminifu kutoa huduma bila upendeleo wa kuangalia rafiki, kabila na rangi ili kuleta usawa katika kuhudumia wagonjwa,” amesema Mtawa.

Naye Ofisa Uhusiano wa TNMC, Ezekiel Nyalusi, amesema ni muhimu jamii ikafahamu haki na wajibu wa mteja au mgonjwa pindi anapofika kupewa huduma za afya katika kituo cha kutolea huduma.

Amezitaja haki hizo kuwa ni kupatiwa taarifa unazohitaji kuhusu ugonjwa na matibabu, Kupatiwa matibabu bila kukemewa, kukaripiwa au kufedheheshwa, kupata huduma kwa wakati, kutegemea aina ya huduma na kuwa na hiyari kupata taarifa zako za kiafya.

Nyingine ni kupata huduma stahiki kwa makundi maalumu kama vile walemavu, wazee, wajawazito, watoto wa chini ya miaka mitano na wenye magonjwa sugu.

Vilevile kulalamika au kutoa mrejesho wa huduma uliyopatiwa, kufuata kanuni na taratibu za kituo husika, kuwaheshimu watoa huduma ikiwa ni pamoja na kutumia lugha safi, kumueleza muhudumu wa afya taarifa zote ambazo zitamuwezesha kutoa tiba sahihi ikiwa ni pamoja na kumpa rekodi za matibabu ya awali ulizonazo na kutafuta matibabu kwa haraka ili wahudumu waweze kukupa huduma sahihi.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora TNMC, Irene Chilewa, amesisitiza wauguzi na wakunga kufuata kanuni za maadili ya uuguzi na ukunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles