30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wauguzi, madaktari wagoma Butimba

Na Clara Matimo, Mwanza

MADAKTARI na wauguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ya Butimba, wamegoma kutoa huduma kwa saa tano wakitaka kuhakikishiwa usalama wao wakati wa kutoa huduma kutokana na baadhi ya wananchi kuvamia hospitali hiyo na kuwazomea wakiwaita wauaji.

Mgomo huo ulianza jana saa 2:30 asubuhi hadi saa 5 baada ya wananchi kuvamia hospitali hiyo na kuanza kutoa lugha za vitisho kwa madaktari na wauguzi wakiwazomea na kuwaita wauaji jambo lililosababisha wasitishe kuendelea kutoa huduma kwa kuhofia kudhuriwa.

Ilielezwa kuwa wakati wakiwazomea wauguzi hao na madaktari, wagonjwa na ndugu wa wagonjwa waliofika hospitalini hapo walianza pia kuwashinikiza kuwatibu haraka, huku wakiwazuia kuwahudumia kwanza wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura huku wakitamka kaulimbiu ya Serikali awamu ya tano ya ‘Hapa Kazi tu’.

Kutokana na wauguzi na madaktari kusitisha huduma kwa wagonjwa, taarifa zilimfikia Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga ambaye alifika mapema hospitalini hapo kwa ajili ya kuzungumza na wagonjwa, madaktari na wauguzi ili kuhakikisha hali ya amani inarejea na wagonjwa wanaendelea kupatiwa matibabu kama kawaida.

Wakielezea malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya, Ofisa Muuguzi Msaidizi, Theonestina Revelian, alisema tangu daktari mmoja, wauguzi wawili na dereva wa hospitali hiyo wasimamishwe kazi kutokana na vifo vya watoto pacha waliofariki muda mfupi baada ya kuzaliwa, wananchi wamekuwa wakiwaita wauaji huku wakiwazomea kwa maneno ya ‘hapa kazi tu’.

“Mkuu leo nilikuwa nahudumia wajawazito, ghafla akaja mama mmoja ambaye na yeye ni mjamzito, akaniambia nesi najisika vibaya sana nahisi naweza kuanguka, ikabidi nimpime nikakuta ana BP (shinikizo la damu) kati ya 200 kwa 180, nikakimbia kwa daktari ambaye alinieleza kumpeleka kwake.

“Lakini cha ajabu nilipokuja kumchukua huyo mama ili nimpeleke kwa daktari, wajawazito wengine sita wakasimama wakaziba njia wakasema huwezi kumpeleka kwa daktari, tunafuata foleni, nikawaambia sawa wote mnahitaji kuhudumiwa, lakini huyu anahitaji matibabu ya dharura, wakakataa na kuanza kunizomea kuwa ‘wauaji nyie mmezoea kutuua’ nikatoka,” alisema.

Revelian alisema kaulimbiu ya Serikali ya awamu ya tano ni nzuri, lakini bahati mbaya wananchi wameipokea vibaya kwa kuwa tangu Jumatano ya wiki iliyopita wenzao waliposimamishwa kazi, wagonjwa wamekuwa wakiwashambulia kwa maneno, huku wakiitumia ‘Hapa Kazi tu’ hali ambayo sasa inawawia vigumu kutoa huduma.

Naye Dk. Diamond Mbukwa, alisema wanasikitika kwa kuwa fani yao ni nzuri, lakini imeingiliwa na wanasiasa kwa kuwa viongozi wanapofika hospitalini kunapokuwa na tatizo, wataalamu wa masuala ya afya hawapewi nafasi ya kusikilizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles