Na ASHA BANI
MAUAJI katika Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, yameendelea kutokea tena baada ya watu watatu kuuawa kwa kupigwa risasi saa nane ya usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo lililotokea Kijiji cha Nyamisati, wilayani humo, ni mwendelezo wa matukio ya mauaji mkoani humo yaliyotokea kwa kufuatana ndani ya kipindi cha wiki moja, baada ya watu wengine wanne kuuawa, mmoja kutekwa na mwingine kujeruhiwa kwa risasi na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wakazi wa Kibiti, wauaji hao waliwaua wanakijiji na kutokomea na miili yao mahali kusikojulikana.
Taarifa hizo zinasema kuwa, wanaodaiwa kupoteza maisha ni Hamid Kidevu, Yahya Makame na Moshi Machela.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamuhusein Kifu, alisema yeye amejulishwa na wananchi kuwa tukio hilo lilitokea saa nane usiku, baada ya watu hao wasiojulikana kufika katika nyumba za wanakijiji hao na kuwaua kisha wakazichukua maiti na kuondoka nazo.
“Nimeelezwa hivyo kwamba majirani walisikia milio ya risasi na kuona wenzao waliopigwa risasi na wauaji wakitokomea na miili hiyo, lakini tayari polisi wamekwenda eneo la tukio na wanaendelea kuwasaka kuhakikisha wanawapata na miili inapatikana,’’ alisema Kifu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, aliliambia MTANZANIA Jumamosi jana kwa njia ya simu kuwa ana taarifa za watu waliouawa katika tukio hilo kuwa ni wawili, akiwamo mwanamke mmoja ambaye naye maiti yake ilichukuliwa na wauaji hao.
Lyanga alisema askari wapo katika eneo la tukio wanawasaka wauaji hao.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Kiislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Hamis Mataka, alisema kitendo hicho ni cha kulaaniwa na hakuna dini yoyote inayopenda uhai wa mtu kutolewa.
Alisema hata wao viongozi wa dini wamechanganyikiwa kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kuibuka siku hadi siku, huku chanzo chake hakijulikani.
“Katika mwezi huu wa Ramadhani tunamuomba Mungu kuondoa kadhia hii inayoendelea ili kila mtu aendeleze funga na kuomba Mungu mabaya haya yasitokee kabisa,” alisema.
Alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama vijitahidi kujua chanzo cha mauaji hayo.
“Hakuna tukio kama hilo liweze kutokea bila kuwa na sababu, ni lazima kuna sababu yake, basi tunamuomba Mungu aweze kubadilisha roho za hao watu ziwe njema na waweze kuthamini roho za wengine,’’ alisema.
Tangu mauaji hayo yatokee, inadaiwa kuwa watu takriban 38 wameshapoteza maisha.
Baada ya mauaji hayo kuendelea kutokea mfululizo mkoani humo, Rais Dk. John Magufuli alifanya mabadiliko ya kumuondoa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, katika nafasi hiyo na kumteua Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuwa IGP mpya.
Baada ya kuteuliwa, Sirro, aliweka mikakati ya kuwabaini wauaji hao na kuwachukulia hatua na siku tatu zilizopita alifika mkoani humo na kuzungumza na wazee ili kujua kiini cha mauaji hayo.