Na RAYMOND MINJA, IRINGA
VIJANA 15 wilayani Kilolo mkoani Irinbga, wametunukiwa vyeti vya pongezi baada ya kufanikiwa kuupata mwili wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Lutangilo, Frank Kastiko, aliyefariki dunia hivi karibuni kwa kusombwa na maji ya Mto Lukosi.
Akiwatunuku vyeti vijana hao, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asiah Abdallah aliwapongeza kwa kujitolea kutafuta mwili wa marehemu.
“Kutokana na taarifa niliyoipata kuhusu mto na ajali ya mwanafunzi huyo, hakuna shaka kwamba kazi mliyofanya ya kuutafuta mwili wa kijana mwenzenu ilikuwa ngumu na ya uungwana,”alisema.
Mkuu wa shule hiyo, Sebastian Chaula alisema mwanafunzi huyo alikutwa na ajali hiyo ya kufamaji jioni ya Julai 29, mwaka huu wakati yeye pamoja na wanafunzi wenzake watatu walipokwenda katika mto huo kufua.
Alisema wakati wanafunzi hao wakifua ghafla mwenzao huyo alivutwa na maji hayo na kupotea.
Chaula alisema ingawa taarifa ya kupotea mwanafunzi huyo ilitolewa, watu wengi walikuwa wakiogopa kuingia katika mto huo unaodaiwa kuwa na mambo ya ushirikina.
“Ndipo walipojitokeza vijana hao 15 na bila woga wakaifanya kazi hiyo hadi kesho yake saa 8.00 mchana walipoupata mwili wa mwanafunzi huyo,” alisema.
Akizungumzia mambo ya ushirikina yanayoelezwa kuwapo katika mto huo, Ackles Ngonyani ambaye ni mmoja wa vijana walioshiriki kuutafuta mwili huo, alisema; “Taarifa za miaka mingi kijijini Kiwalamo zinasema mto huo ni wa ajabu na una mambo ya ushirikina.”
Ngonyani alisema mto huo ambao maji yake ni ya baridi kama seruji, unadaiwa kuwa na nyoka wa ajabu mwenye vichwa 12 jambo linawaogopesha wananchi wengi wa kijiji hicho na maeneo jirani.
Alisema Ili kuepukana na maajabu hayo, walilazimika kupata maombi kutoka kwa wachungaji wa kijiji hicho kabla ya kuanza kuutafuta mwili wa mwanafunzi huyo.
Vijana hao walimshukuru mkuu wa wilaya kwa kutambua mchango wao katika jamii huku wakiahidi kufanya mengine mema.