23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi wengi Tazara kustaafu kwaleta kilio

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WASTANI wa wafanyakazi 400 wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) wanastaafu kila mwaka na kusababisha kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi.

Akizungumza jana wakati ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ulipotembelea shirika hilo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tazara, Geoffrey Sengo, alisema shirika hilo lililoanzishwa likiwa na wafanyakazi 7,000 hivi sasa lina wafanyakazi 2,775.

Alitoa mfano wa baadhi ya watumishi waliopo idadi yao na umri wao kwenye mabano ni 338 (miaka 55 – 60), 300 (51 – 55), 324 (46 – 50) na 470 (36 – 41).

“Wafanyakazi wengi wako katika umri wa kustaafu na kwenye soko kuna changamoto, unaweza kupata mtu ana ‘mechanical engineering’ lakini hana uzoefu kwenye sekta ya reli,” alisema Sengo.

Kwa upande wake, Mkuu wa NIT, Profesa Zacharia Mganilwa, alilishauri shirika hilo kutoa nafasi za kujitolea kwa wahitimu wa fani mbalimbali kama njia ya kukabili uhaba huo.

“Tuna vijana wengi sana ambao wamehitimu na hawajapata kazi, hivyo Tazara wangeweza kutoa nafasi ya kuja kujitolea.

“Kwenye chuo chetu cha usafirishaji tunao wanaomaliza ‘mechanical engineering’, ‘automobile engineering’, maafisa usafirishaji ukiwemo usafiri kwa njia ya reli, tunao wanaochukua shahada ya masuala ya fedha katika usafirishaji, masoko na utawala pia.

“Wakipewa fursa ya kujitolea yawezekana katika kipindi hicho cha kujitolea miezi sita mpaka mwaka mmoja wakawa na mawazo mapya yakasaidia shirika la Tazara,” alisema Profesa Mganilwa.

Pia alilishauri shirika hilo kuwapelekea baadhi ya changamoto walizonazo ili walimu na wanafunzi wazifanyie utafiti utakaowezesha kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa NIT, Profesa Bavo Nyichomba, alisema ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujifunza namna wanavyoweza kushirikiana na shirika hilo kuwezesha kupata wataalamu wa nyanja mbalimbali wanaozalishwa na chuo hicho.

“Tazara inashughulika na masuala ya usafiri na sisi NIT ndiyo maeneo yetu, kwahiyo lengo letu ni kuangalia maeneo gani tunaweza kushirikiana, kwa sababu tunatoa wanafunzi kwenye maeneo haya,” alisema Profesa Nyichomba. 

Alisema wamebaini shirika hilo linahitaji mainjinia, mafundi na wataalamu wengine wa fani tofauti, hivyo wataichangamkia fursa hiyo kwa sababu tayari wanatoa wanafunzi wa kutosha.

Kwa mujibu wa Profesa Nyichomba, zaidi ya wahitimu 1,500 wanahitimu katika chuo hicho kila mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles