Na BEATRICE MOSSES
-MANYARA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara imewafukuza kazi watumishi wake watano, huku wengine wakionywa kwa makosa ya utoro kazini.
Watumishi waliofukuzwa wanne kati yao ni wa idara ya afya na mmoja ni mtendaji wa kijiji.
Akitoa taarifa jana mjini hapa katika Baraza la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, George Bajuta amewataja waliofukuzwa kazi kuwa ni Dorath Aidan, Gisela Kweka, Sophia Kashatila na Elia Mugeta ambao wote ni wahudumu wa Idara ya Afya katika Hospitali ya wilaya pamoja na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Gidika, Cresent Nada.
Alisema uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi hao ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kilichokutana Julai 20, mwaka huu na baadaye kupata baraka za Baraza la Madiwani.
“Sio kazi ya Baraza la Madiwani kuwafukuza kazi watumishi, hii ni hatua ya mwisho kabisa baada ya jitihada zote za kuwatafuta kushindikana,” alisema Bajuta.
Wakati huo huo baraza hilo limetoa omyo kwa watumishi wengine wanne na kuridhia wakurudishwe kazini baadaya kukamilika kwa mashauri yao.
Waliopewa onyo na kurejeshwa kazini ni Gisela Kweka mhudumu wa afya, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Daraja III, Alexander Ngeni, Ofisa Mtendaji wa Kijiji Daraja la III, Peter Darema pamoja na aliyekuwa Mratibu wa TASAF Wilaya, Stephen Samhenda ambaye amerudishwa kwenye nafasi yake.
Wengine ni Mtumishi Maulid Kiwanga Afisa mtendaji wa kijiji daraja III ambaye hakupatikana na hatia na Ester Bura Tluway ambaye ni Ofisa Mtendaji Daraja la III ambaye shauri lake halijakamilika.