Watumishi watano TRC wafariki ajalini

0
746

Mwandishi Wetu

Watumishi watano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wamefariki dunia baada ya treni ya uokoaji kugongana na kiberenge katika eneo la kati ya Stesheni za Mwakinyumbi na Gendagenda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC leo Jumatatu Machi 23, ajali hiyo iliyohusisha watumishi sita imetokea jana Jumapili Machi 22, ambapo wanne walifariki papo hapo na majeruhi wawili walifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magunga, Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya kupatiwa matibabu, ambapo majeruhi mmoja alifariki akipatiwa matibabu hospitalini hapo na kufanya idadi ya waliofariki kufikia watano.

Waliofariki katika ajali hiyo wametajwa kuwa ni Ramadhani Gumbo, Injinia Fabiola Moshi, Joseph Komba, Philip Kajuna na George Urio.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa shirika hilo, Jamila Mbarouk amesema uchunguzi wa kujumuisha kwa kushirikiana na taasisi nyingine utafanywa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here