Na SEIF TAKAZA -SINGIDA
SERIKALI imeonya watumishi wa umma kujiepusha na mambo ya siasa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, ambapo wale watakaokwenda kinyume na agizo hilo watachukulia hatua kwa mujibu wa kanuni, sheria na utaratibu wa kazi.
Onyo hilo lilitolewa juzi mjini Singida na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Serikali, ambapo alisema kuwa watumishi wa umma hawakupata ajira zao serikalini kwa ajili ya siasa, na wala si wanasiasa.
Alisema hawatakiwi na hawawajibiki kujihusisha na mambo ya siasa ili kuepuka kujiingiza matatani na serikali inayowaongoza.
“Wajibu wa mtumishi wa umma ni kutoa ushauri wa kitaalamu mambo mengine ya kisiasa hasa kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, mtuachie wenyewe wanasiasa. Sisi watumishi wa umma tuendelee kutoa huduma sahihi kwa mujibu wa mikataba yetu,” alisema Dk. Mwanjelwa
Pamoja na hali hiyo alitoa agizo kwa wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya nchini, kujenga tabia ya kufanya mikutano ya mara kwa mara na watumishi wao, ili kuimarisha upendo, amani na mshikamano katika sehemu ya kazi.
“Nawaomba sana, mikutano hii itumike kusikiliza kero na changamoto zenu na kuzipatia majibu yake, kwani itasaidia pia kuondoa dosari ndogondogo za watumishi, badala ya kumsubiri waziri au kiongozi mwingine wa ngazi ya juu, aje kutoa jibu,” alisema.
Aliwataka wakurugenzi kuwajali na kuwapenda watumishi wenzao wa umma, lengo likiwa kuwasaidia na kudumisha utamaduni wa kufanya kazi kama timu moja yenye nia moja ya kupata ushindi, kwa jili ya kumpatia mwananchi huduma bora.
“Na ninyi watumishi wa umma, nawaomba mpendane na mjali kazi zenu, tendeni haki!, chezea mshahara ila usichezee kazi. Kazi ni fursa adimu sana kwa maisha yako. Hakikisheni mnazingatia sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa ili kuilinda kazi,” alisisitiza.
Akizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Dk. Mwanjelwa, alisema kuwa katika awamu inayofuata, utakuwa umeboreshwa zaidi na unatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote na Rais Dk. John Magufuli.
Alisema walengwa watakaonufaika na fedha za ruzuku ya Mfuko wa TASAF iliyoboreshwa, wahakikishe wanatumia vema fedha hizo kwa kuwekeza kwenye masua;a ua uchumi kwani ndiyo lengo lililokusudiwa na Serikali.