Na ABDALLAH AMIRI, IGUNGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, imewakamata watumishi watatu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Iguwasa) kwa tuhuma ya kutumia maji pasipo kulipia kwa zaidi ya miaka sita.
Meneja wa Idara ya Maji, Wilaya ya Igunga, Raphael Merumba, aliwataja watumishi waliokamatwa kuwa ni Augustina Ernest, Deus Mgeta na Maiko Kafunda, wote watumishi wa Iguwasa.
Melumba alisema watumishi hao walikamatiwa ofisini kwake, juzi asubuhi. “Maofisa hao wa Takukuru waliongozwa na Kamanda wao wa wilaya, Warioba Msena.
“Baada ya kuwakamata hapa ofisini, waliondoka nao hadi nyumbani kwao na waliposoma mita za maji, walibaini watumishi hao hawajawahi kulipia tangu wavute maji majumbani mwao kwa miaka mingi.
“Nilipoambiwa hawajawahi kulipia bili za maji kwa muda wote huo na mimi nilifuatilia kwa kusoma mita zao ndipo nilibaini wizi huo wa miaka mingi.
“Mbali na hao, nilibaini mwingine aliyebainika kuiba maji ni Ambangile Enock ambaye naye hajawahi kulipia maji.
“Kwa hiyo, tayari wahusika wameandikiwa barua wakitakiwa kujieleza ndani ya siku tatu kabla hawajachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisema Merumba.
Kwa upande wao, watumishi hao walipozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, walikiri kutolipia maji kwa miaka mingi.