25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa zaidi wachangamkia msamaha wa JPM

KULWA MZEE na JANETH MUSHI-DAR es salaam/ARUSHA

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kuongeza siku saba kwa watuhumiwa wa utakatishaji fedha na uhujumu uchumi kukiri makosa yao na kulipa fedha hizo ili waachiwe, baadhi wameanza kufikishwa mahakamani na kukiri huku wengine wakiendelea kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Waliofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kukiri ni wafanyabiashara Magdalena Uhwello na Halima Nsubuga.

Wafanyabiashara hao walikiri makosa ya kutakatisha fedha na wamehukumiwa kulipa Sh milioni 101 na Dola za Marekani 388,000 kutaifishwa na Serikali.

Mahakama imeamuru washtakiwa wakishindwa kulipa  fedha hizo wataenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kuendesha upatu na miaka 20 kwa kutakatisha fedha.

Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo alisema baada ya washtakiwa kukiri makosa hayo na mahakama kuwatia hatiani, watapaswa kulipa faini ya Sh milioni moja au kifungo jela mwaka mmoja kwa kosa la kufanya biashara ya upatu.

Alisema mahakama imewapa adhabu katika mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo watatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 100 au kifungo jela miaka 20.

Hakimu Mwaikambo alisema washtakiwa wakishindwa kulipa faini hiyo, adhabu itakwenda kwa pamoja, hivyo watatakiwa kutumikia adhabu ya miaka 20 jela.

Mahakama ilikubali maombi ya Jamhuri ya kutaifisha fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya washtakiwa na kuwa mali ya Serikali.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wanaotaka kujiingiza katika biashara hiyo na kuomba mahakama itaifishe fedha hizo.

Wakili wa Utetezi, Augustine Shio, aliomba mahakama iwaonee huruma washtakiwa hao kwa sababu ni kina mama ambao wana watoto wadogo wanaowategemea na hawana kipato chochote.

Alidai mahakama izingatie kukubali kosa kwa washtakiwa kumeondoa usumbufu kwa mahakama, kuokoa gharama za kesi kufanya upelelezi kwenda Uganda na kwamba ni wakosaji wa kwanza, hivyo itoe adhabu ya faini katika makosa yote.

Fedha zilizotaifishwa na kuwa mali ya Serikali ni Dola za Marekani 124,433 zilizopo kwenye akaunti ya Benki ya Equity Tanzania na Dola za Marekani 263,567 zilizopo kwenye akaunti ya Equity Uganda.

Katika mashtaka ya kwanza, inadaiwa Aprili Mosi, 2017 na Juni 30, 2017 maeneo ya Dar es Salaam washtakiwa hao walikula njama kutenda kosa la kusimamia na kuendesha biashara ya upatu.

Kwamba walikusanya fedha kutoka kwa watu mbalimbali ambazo walikuwa wakichangia kwa kuwaahidi kuwapatia faida watakayopata.

Inadaiwa Aprili 25, 2017 washtakiwa hao walitakatisha fedha. Wanadaiwa walificha chanzo halisi cha fedha haramu, walihamisha Dola za Marekani 263,567 kwenda katika akaunti ya Equity Uganda inayomilikiwa na Magara huku wakijua zimetokana na zao la uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles