29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Watu wenye ulemavu na kizungumkuti cha asilimia 3 ya ajira

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

“Nina mfano wa mtu mmoja aliwahi kuambiwa wewe uko hivyo (yaani mwenye ulemavu wa macho) utawatisha wateja wetu, mwingine alikuwa mwenye ualbino naye alikataliwa akaambiwa hawezi kazi ya garden,” anasema Omary Itambu ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wasioona Tanzania (TAB).

Itambu anasema yeye pia aliwahi kuomba kazi ya uelimishaji rika katika Shirika moja la kimataifa hakuwahi kupata licha ya kuwasilisha vyeti vilivyohitajika.

Joyce Jumbe mwenye uziwi anatafuta ajira tangu alipohitimu chuo kikuu na changamoto kubwa anayokutana nayo ni kutokuwepo kwa mkalimani wa lugha ya alama anapoitwa kufanya usaili wa nafasi mbalimbali za kazi.

Itambu ni mfano wa watu wengi wenye ulemavu ambao wamekuwa wakisaka ajira bila mafanikio licha ya kuwa na sifa zinazohitajika katika kazi husika wanazoomba.

Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010 inaelekeza unapoajiri wafanyakazi zaidi ya 20 katika taasisi za umma au binafsi asilimia tatu wanapaswa wawe wenye ulemavu lakini bado kumekuwa na utekelezaji usioridhisha wa sheria hiyo.

“Angalau kidogo Serikali inajitahidi lakini shida bado iko kwenye sekta binafsi, kwahiyo tunaomba wale wote waliokuwa na mamlaka wawabane waweze kutekeleza jukumu la asilimia tatu. Tutafurahi kwa sababu ni haki na ni wajibu wa nchi na viongozi kusimamia matakwa ya kimataifa ili kuwaweka watu wenye ulemavu kuwa na haki sawa kwani wao ni binadamu kama wengine,” anasema Itambu.

Itambu anasema wapo wasioona na watu wengine weye ulemavu wana sifa na vigezo vya kufanya kazi mbalimbali lakini wakienda kuomba ajira wanakosa.

“Sijui wapi Serikali inakwama kwa sababu tulikuwa tukililia watu wenye ulemavu kuingia kwenye ngazi za maamuzi sasa tunao kwahiyo wapaze sauti ili hizi sheria zitekelezwe.

“Niombe kwa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa salamu aliyoitoa na sisi kuitikia kazi iendelee, ni wakati sasa umefika kuifanya kazi iendelee kwa kutimiza yale ambayo sheria ya kimataifa inazitaka nchi wanachama kutekeleza hasa kwa watu wenye ulemavu,” anasema.

Naye Joseph Migila ambaye ni Meneja Mipango wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), anasema bado kuna changamoto ya usimamizi wa sheria hiyo hasa katika kufuatilia utekelezaji wake.

“Hata tukiamua kufanya sensa sasa hivi yapo mashirika mengi hapa Tanzania yameajiri watu zaidi ya 20 lakini je, asilimia tatu ya watu hao ni wenye ulemavu,”? Anahoji Migila.

Anasema pia ufikikaji wa taarifa za nafasi mbalimbali za kazi nayo ni changamoto kwani nyingi zinatangazwa kwenye mitandao, televisheni na magazeti.

“Mfano kwenye gazeti tangazo linaandikwa kwa maandishi madogo ambayo mtu mwenye uoni hafifu hawezi kusoma, kwahiyo unyanyapaa unaanzia kwenye tangazo.

“Unakuta mtu ni kiziwi na kuna taarifa ya nafasi za kazi inatolewa kwenye televisheni lakini hakuna mkalimani wa lugha ya alama,” anasema.

Anasema pia waajiri wengi wamekuwa hawaajiri watu wenye ulemavu kwa sababu wanaogopa kuingia gharama za kuwapatia mahitaji ya muhimu ili waweze kufanya kazi kulingana na ulemavu walionao.

“Unapomuajiri mtu mwenye ulemavu wakati mwingine anakuja na changamoto ambazo kimsingi lazima zitatuliwe ili aweze kufanya kazi, mfano umemuajiri mtu mwenye ulemavu wa macho wana mahitaji ya kutumia nukta nundu au kompyuta zenye sauti kwahiyo imekuwa pia ni changamoto,” anasema.

Migila anasema wanaendelea kujenga ushawishi na utetezi kuhakikisha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya Mwaka 2010 inatekelezwa kwa vitendo.

“Hapa Shivyawata tuko vyama 10 ambavyo vinawakilisha aina mbalimbali za ulemavu hivyo, tunapotoa ushawishi na utetezi katika kazi tunazozifanya tunawaeleza kwamba unapokuwa na mtu mwenye ulemavu wa macho au ualbino ni vitu gani anahitaji ili mwajiri ampatie aweze kufanya kazi katika mazingira rafiki,” anasema Migila.

Hata hivyo licha ya changamoto kadhaa, Migila anakiri kuwa uelewa wa masuala ya watu wenye ulemavu unaongezeka na kwamba hali hiyo inachagiza kuendelea kutambulika na kuondoa dhana ya unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu.

Meneja huyo anashauri wakati wa usaili wa nafasi mbalimbali za kazi mazingira yawe rafiki ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kufanya usaili bila vikwazo.

“Umma unatakiwa kujua kwamba watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii na wanastahili kupata fursa zote zinazotokea nchini hivyo, jamii iondoe dhana ya unyanyapaa na kutambua haki na masilahi ya watu wenye ulemavu,” anasema.

Naye Joyce Jumbe (31) ambaye ni kiziwi na mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Jamii na Uongozi kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), anasema aliwahi kuomba kazi sehemu tano tofauti na kote huko hakukuwa na mkalimani wa lugha ya alama wakati wa usaili.

Anasema alikuwa akifanya usaili kwa kuandika au kujibu maswali baada ya kumuangalia usoni yule anayemuuliza.

“Niliomba kazi ya Social Worker Muhimbili nikaitwa kwenye ‘interview’ iliyofanyika DUCE. Hakukuwa na mkalimani lakini nilijieleza kuwa nina matatizo ya kusikia, walinipa karatasi nikaandika majibu ya maswali waliyoniuliza… nilianguka kwenye hatua ya kwanza ya ‘interview’ sikuingia hatua ya pili.

“Kwingine nilikwenda unakaa unamuangalia usoni HR (Human Resource) anakuuliza unajibu, interview inataka utulivu kuna mengine unajibu sivyo ulivyoulizwa kumbe tayari nimekosa sifa…nashindwa si kwa kupenda ni kwa sababu ya kutokuwa na mkalimani,” anasema Joyce.

CHAMA CHA WAAJIRI

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, anasema suala la kuajiri watu wenue ulemavu bado ni changamoto kama nchi lakini wanaendelea kuwahamasisha wanachama wao kutekeleza sheria hiyo.

“Utekelezaji wa sheria unataka msukumo, hatukatai ndiyo maana tunaishukuru Serikali kwa sababu tunaona kuna mawaziri, makatibu wakuu wenye ulemavu. Na sisi katika kuhamasisha hilo kila mwaka huwa tunatoa tuzo kwa mwajiri bora aliyeajiri watu wenye ulemavu na mwaka huu pia tutatoa Desemba,” anasema Dk. Mlimuka.

Dk. Mlimuka anasema pia wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu na kuwahamasisha kuomba kazi.

MIPANGO YA SERIKALI

Kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 Serikali inatarajia kuajiri watumishi 44,096 wa kada mbalimbali kama za afya, elimu, kilimo, uvuvi, polisi, magereza, zimamoto na uokoaji na uhamiaji.

Hata hivyo katika ajira hizo haijaainishwa watu wenye ulemavu wataajiriwa wangapi.

Aidha Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, anasema wanaendelea kuwahimiza watu kuzingatia sheria hiyo kuepuka kutiwa hatiani.

Anasema pia wana mpango wa kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya kazi ili kuona kama kuna uzingatiwaji wa sheria hiyo.

Kulingana na sheria hiyo, adhabu kwa anayeikiuka ni kifungo cha miaka miwili jela, faini ya Sh milioni mbili au adhabu zote kwa pamoja.

“Hatutaki tufike kwenye kufungana ndiyo maana tunaendelea kujengeana uwezo na kuweka msisitizo ili kuwe na uzingatiwaji wa sheria hii,” amesema Nderiananga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles