Clara Matimo- Mwanza
WATU 98 kati ya 330 waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa afya zao kwa hiari katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando(BMC) jijini Mwanza wamekutwa na maambukizi ya magonjwa mbalimbali, ikiwamo wa homa ya ini.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa BMC, Profesa Abel Makubi, wakati akizungumzia uzinduzi wa wodi maalumu na za kulipia (binafsi) uliyoenda na utoaji wa huduma ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, ikiwemo kisukari, homa ya ini na shinikizo la juu la damu (Hypertension) kwa wakazi wa kanda ya ziwa.
“Idadi hii, ni sawa na asilimia 28.8 ya watu 330 tuliowapima, 20 sawa na asilimia sita wamekutwa na maambukizi ya homa ya ini, 16 sawa na silimia 4.8 wana dalili za ugonjwa wa kisukari na 62 sawa na asilimia 18, wamekutwa na shinikizo la juu la damu,” alisema Professa makubi.
Kuhusu uzinduzi wa wodi hizo, Profesa Makubi alisema mafanikio yametokana na mapato ya ndani ambapo zaidi ya Sh milioni 300 zimetumika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo.
“Baadhi ya wodi, ni mpya tumejenga, pia tumefanya ukarabati wa baadhi ya majengo kutokana na maboresho haya chumba cha maalumu chenye vitanda viwili kuna vitu kama runinga, internet na kengele ya kumuita mhudumu, itagharimu Sh150,000 kwa siku, vyumba vya binafsi vyenye vitanda viwili vya wagonjwa Sh 50, 000 kwa siku na vyumba vyenye wagonjwa watano ni Sh 35, 000 kwa siku,”alisema.
Daktari bingwa wa mfumo wa chakula na ini wa BMC, Hyasinta Jaka alisema maambukizi ya ugonjwa wa ini yanatokana na mwingiliano wa majimaji ya mwilini kama mate, jasho na hata kujamiiana.
Mmoja wa wananchi waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi, Anitha Kato, aliishukuru hospitali hiyo kwa kutoa huduma ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali bure.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na BMC kuboresha huduma mbalimbali kwa manufaa ya wananchi pia aliipongeza kwa kuboresha huduma za kibingwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa hospitali hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande, alisema uzinduzi wa wodi hizo na huduma zingine zinazotolewa hospitalini hapo ni moja ya wajibu wa kanisa hilo katika kutoa huduma ya uponyaji kwa binadamu wote bila kujali dini, kabila wala utaifa.