‘WATU 24 KATI YA 100 WAACHA ARV’S’

0
665

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WATU 24 kati ya 100 wamebainika kuacha kutumia Dawa za Kufubaza Makali ya VVU (ARV’s).

Hayo yalibainika hivi karibuni Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti ya uhakiki wa muda wa kati wa Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kudhibiti Ukimwi wa 2013/14 hadi 2017/18.

Suala hilo ni miongoni mwa mapendekezo 10 yaliyotolewa na washauri waelekezi waliofanya utafiti huo ambao walishauri mbinu mbalimbali zitumike kuhakikisha wale walioanza dawa hawapotei.

Akizungumza na MTANZANIA, Mshauri Mwelekezi aliyefanya utafiti huo, Dk. Emmanuel Matechi, alisema walibaini watu wanaacha dawa kwa sababu ya umbali mrefu wa vituo vya matibabu, kuhamahama na kupuuzia baada ya kupata nafuu.

“Ndani ya mwaka mmoja utafiti umeonyesha katika watu 100 waliosajiliwa, 76 ndio wanaorudi na takwimu hizi zinajumuisha na wale wanaofariki,” alisema Dk. Matechi.

Alisema unahitajika mkakati maalumu wa kuhakikisha watu waliosajiliwa kutumia dawa hizo wanaendelea na matibabu kama ilivyoelekezwa.

“Tutumie mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa wale walioanza dawa hawapotei. tuwe na mfumo wa kuwatambua popote watakapokuwa,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Justine Mwinuka, alisema katika Wilaya ya Wanging’ombe watu 419 waliacha dawa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za umbali mrefu.

Alitolea mfano wa watu wanaotoka Kijiji cha Wangama kwamba wamekuwa wakitembea kilomita 29 kwenda katika kituo cha huduma kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi (CTC) Kidugala kupata dawa. Katika kijiji hicho watu 18 waliacha dawa.

“Ili ufike CTC Kidugala unaweza kutumia usafiri wa bodaboda, basi, ama kutembea kwa miguu, lakini wakati mwingine mtu anakosa nauli ama anakuwa amechoka anaamua kuacha dawa,” alisema Mwinuka.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, takwimu hizo walizipata kupitia kwa watetezi wa afya ya jamii wanaofanya kazi vijijini ambao wako chini ya Nacopha.

Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Richard Ngilwa, alisema wamejipanga kutafuta fedha za ndani na kuacha kutegemea wafadhili katika utekelezaji wa afua mbalimbali za Ukimwi.

“Mapendekezo yote yaliyotolewa tutayapeleka kwenye kikao kingine cha wadau ambacho hufanyika kila robo mwaka na baadaye kutakuwa na ripoti ya kina,” alisema Ngwila.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here