27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Watswana wavutiwa na matumizi ya TEHAMA katika Taasisi ya OSHA

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wataalam kutoka Ofisi ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Botswana wamefanya ziara katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kujifunza jinsi Taasisi hiyo inavyotumia mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa masuala ya Afya na Usalama mahali pa kazi.

Meneja wa Afya wa OSHA, Dk. Jerome Materu akikabidhi zawadi kwa Kaimu,Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Botswana, Gopolang Maakwe mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea ofisi za OSHA Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Serikali wa Botswana, Gopolang Maakwe, nchi yake ipo katika mchakato wa kutengeneza mfumo wake wa ofisi mtandao kwa ajili ya kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.

Akizungumza alipotembelea Ofisi za OSHA na kufanya kikao na menejimenti hivi karibuni, amesema wameona ni muhimu kujifunza kwa nchi ambazo zimepiga hatua katika matumizi ya mifumo hiyo.

“Tumekuja hapa kujifunza namna ambavyo Tanzania imefanikiwa kujenga na kutumia mfumo wa ofisi mtandao katika Taasisi zake zaidi ya 200. Tuliposikia kwamba Tanzania wamefanikiwa katika eneo hili tukaona ni vyema akawa mshirika wetu katika zoezi lililopo mbele yetu la kuhakikisha kwamba Serikali nzima ya Botswana inaingia katika matumizi ya ofisi mtandao kuanzia mwaka 2024/2025,” amesema Maakwe.

Ameongeza kuwa: “Katika ziara yao wamefurahi kusikia kwamba mfumo unaotumika Tanzania umeandaliwa kwa kutumia wataalam wa ndani hivyo hata uangalizi na matengenezo yake hayatakuwa na gharama kubwa kwani mara nyingi uundaji wa mifumo ya TEHEMA umekuwa ukitegemea watoa huduma wa nje ya serikali jambo ambalo limekuwa likiongeza gharama za uendeshaji.”

Aidha, ameishukuru OSHA na serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa ukarimu wao na ameahidi kwamba wataendelea kuja kujifunza zaidi hadi hapo watakapokamilisha mfumo wa nchi yao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa OSHA, Dk. Jerome Materu, amemshukuru Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Taasisi ya OSHA kutumia mfumo wa ofisi mtandao na mifumo mingine ya serikali ambayo imesaidia kuongeza ufanisi katika utendaji wa OSHA.

“Mfumo wa ofisi mtandao pamoja na mifumo mingine iliyoandaliwa na serikali yetu imesaidia sana kupunguza urasimu na kutuongezea kasi ya kuwahudumia Watanzania. Sisi kama OSHA tunao mfumo wetu wa ndani wa Usimamizi wa Taarifa za maeneo ya kazi nchini ujulikanao kama WIMS ambao tunautumia sambamba na mfumo wa ofisi mtandao na mifumo mingine ya serikali katika kuwahudumia wadau wetu,” alieleza Dk. Materu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Huduma za Usalama na Afya, kabla ya kuanza kutumia mifumo hiyo kulikuwa na changamoto katika upatikanaji wa huduma za OSHA ambapo cheti cha usajili wa eneo la kazi kilikuwa kinapatikana baada ya siku saba huku cheti cha kukidhi viwango vya usalama na afya kikiandaliwa kwa mwezi mzima.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Botswana, Gopolang Maakwe pamoja na watumishi wa Ofisi yake (waliokaa) wakiwa katikapicha ya pamoja na baadhi ya viongozi katika Menejimenti ya OSHA katika Ofisi za Dar es Salaam.

“Kwasasa mdau anaweza kusajili eneo lake la kazi ndani ya masaa machache na kupata cheti cha kukidhi viwango vya usalama na afya ndani ya siku tatu,” amefafanua Mkurugenzi Materu.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ambayo inasimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Usimamizi wa Sheria hii unahusisha kuyatambua maeneo ya kazi kwa kuyapa usajili na kisha kuyafikia kwa ajili ya ukaguzi na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi kwa minajili ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa mahali pa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles