23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto watatu wenye ulemavu waomba msaada

TUNU NASSOR – MKURANGA

WATOTO watatu wa familia moja wanaoishi Kitongoji cha Mkanze, Kijiji cha Kibururu, Kata ya Kiparang’anda, Mkuranga mkoani Pwani wanahitaji msaada kutoka kwa wahisani kutokana na kuwa walemavu wa kutokutembea na mdomo mzito kuzungumza.

Akizungumza na MTANZANIA, Baba mzazi wa watoto hao, Hamisi Sabili alisema watoto hao walizaliwa wakiwa na afya njema lakini ulemavu huo umeanza kugundulika wakati wa makuzi yao.

Watoto Hawa ambao ni Hamidu Sabili, (19), Husseini Sabili (13) na Shani Sabili (11) hawawezi kujihudumia wenyewe hivyo kuhitaji huduma ya karibu ya jamii yao.

Sabili alisema kila mmoja alipofikia umri wa miezi kumi na moja ndipo waligundua kama wana matatizo hayo.

“Baada ya kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza alikuwa mzima lakini alipofikisha umri wa miezi 11 ndipo tukagundua kuwa na tatizo hilo, hivyo hivyo mtoto wa pili na watatu,” alisema Sabili.

Alisema baada ya kuzaliwa kwa mtoto wa nne naye pia alikuwa na tatizo hilo, lakini bahati mbaya alifariki.

Akiongea kwa msikitiko, Sabili alisema watoto wake wanaishi kwa shida kila kitu wanahitaji kusaidiwa na kusababisha yeye na mkewe kusimamisha shughuli za uzalishaji ili kuwalea watoto wao.

“Wanajisaidia bila kutoa taarifa na tunatambua iwapo tutaona nzi wamewazonga tunajua kuna mmojawapo amejisaidia,” alisema.

Alisema yeye na mkewe hujishughulisha na kilimo, hivyo imefikia wakati wanalazimika kusitisha shughuli zao ili kutoa msaada kwa watoto hao huku wakigawana majukumu ya namna ya kuwahudumia.

Sabili alisema wamekuwa wakipitia wakati mgumu katika maisha kwa kuwa wanapata shida kupata huduma ya chakula, matibabu na huduma nyingine za kibinadamu.

Anawaomba Watanzania kumsaidia kupata huduma za kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi, na hata kupatiwa bima ya afya itakayomwezesha kuimarisha afya za watoto hao.

“Pindi wanapokuwa wanaumwa tunalazikika kuwabeba mgongoni na kutembea umbali mrefu kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga,” alisema Sabili.

Alisema pamoja na mahitaji hayo, pia anaomba msaada wa kuwapatia baiskeli za kuwapeleka shuleni ili waweze kupata elimu.

Sabili alisema yeyote aliyeguswa na matatizo ya watoto hawa anaweza kuwasiliana kwa simu namba 0654499681 au 0788748173 ili kuwasaidia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles