29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto watatu wa familia moja wafariki baada ya kula viazi, maharage pori

Na Walter Mguluchuma-Katavi

WATOTO watatu wa  familia moja waliofahamika kwa majina ya Kabula  Yohana (6), Modesta  MAkoye (4) na  Ezekiel Yohana (3) wakazi wa Kijiji cha  Igongwe Kata ya Stalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda, wamefariki dunia baada ya kula viazi vitamu na mbegu za mmea pori  unaofanana na mahagwe vinavyosadikiwa kuwa na sumu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mko wa Katavi,  Benjamin Kuzaga, vifo vya watoto hao wa familia moja vilitokea hapo  juzi saa 12 jioni kwa nyakati tofauti kijijini  hapo.

 Alisema siku hiyo ya tukio marehemu hao  watatu majira ya mchana wakiwa na watoto wengine watatu ambao ni   Yoha Sabuni, Cristina Yohana na Paulo Yohana,  walichuma mbegu za mmea pori mfano wa kunde na kula pamoja na viazi vitamu vilivyopikwa .

 Alisema baada ya kula hali zao zilibadilika na walianza kuhisi maumivu ya tumbo na wakati huo wazazi  wao ambao ni Yohana Elias na Agnes Lucas,  walikuwa shambani jambo lililofanya watoto wasipate msaada wa haraka.

 Alieleza ilipofika 12:30  jirani yao aitwaye Amos Antony aliwakuta watoto hao wakiwa wamelala chini huku wakiwa wanalalamika maumivu ya tumbo.

 Kutokana na hali ya watoto hao ilipokuwa, aliwakimbiza kwenye Zahanati ya Sitalike  kwa ajili ya matibabu huku hali zao zikiwa zinazidi kuwa mbaya ambapo Kabula  Yohana na Ezekiel Yohana, walifariki Dunia  na ikalazimika mmoja aliyebaki kukimbizwa katika Hospitali teule ya Mkoa wa Katavi .

Kamanda Kuzaga alisema baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitali aliendelea kupatiwa matibabu  na ilipofikia majira ya saa nne  usiku Modessta Makote  naye alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.

 Alisema watoto wawili  ambao ni  Yona   Sabuni  na Cristina  Yohana  bado wamelazwa katika Hospitali Teule ya Mkoa wa  Katavi wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri .

 Aidha  baada   ya tukio hilo  timu ya madaktari walifanya  uchunguzi  wa kitabibu  katika miili ya marehemu wote watatu  na baada ya uchunguzi  kukamilika ilikabidhiwa  kwa ndugu wa marehemu kwajili ya taratibu za mazishi .

Kamanda Kuzaga alisema  hadi sasa  hakuna  mtu yeyote  anaeshikiliwa  na jeshi la polisi  kuhusiana  na  tukio hilo.

Alisema  uchunguzi bado unaendelea kufanyika kuhusiana na tukio hili  ofisi ya Mkemia Mkuu  wa Serikali  ili kubaini aina ya sumu iliyosababisha vifo vya watoto hao .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles