Na Walter Mguluchuma-Katavi
WATOTO watatu wa familia moja waliofahamika kwa majina ya Kabula Yohana (6), Modesta MAkoye (4) na Ezekiel Yohana (3) wakazi wa Kijiji cha Igongwe Kata ya Stalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda, wamefariki dunia baada ya kula viazi vitamu na mbegu za mmea pori unaofanana na mahagwe vinavyosadikiwa kuwa na sumu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mko wa Katavi, Benjamin Kuzaga, vifo vya watoto hao wa familia moja vilitokea hapo juzi saa 12 jioni kwa nyakati tofauti kijijini hapo.
Alisema siku hiyo ya tukio marehemu hao watatu majira ya mchana wakiwa na watoto wengine watatu ambao ni Yoha Sabuni, Cristina Yohana na Paulo Yohana, walichuma mbegu za mmea pori mfano wa kunde na kula pamoja na viazi vitamu vilivyopikwa .
Alisema baada ya kula hali zao zilibadilika na walianza kuhisi maumivu ya tumbo na wakati huo wazazi wao ambao ni Yohana Elias na Agnes Lucas, walikuwa shambani jambo lililofanya watoto wasipate msaada wa haraka.
Alieleza ilipofika 12:30 jirani yao aitwaye Amos Antony aliwakuta watoto hao wakiwa wamelala chini huku wakiwa wanalalamika maumivu ya tumbo.
Kutokana na hali ya watoto hao ilipokuwa, aliwakimbiza kwenye Zahanati ya Sitalike kwa ajili ya matibabu huku hali zao zikiwa zinazidi kuwa mbaya ambapo Kabula Yohana na Ezekiel Yohana, walifariki Dunia na ikalazimika mmoja aliyebaki kukimbizwa katika Hospitali teule ya Mkoa wa Katavi .
Kamanda Kuzaga alisema baada ya mtoto huyo kufikishwa hospitali aliendelea kupatiwa matibabu na ilipofikia majira ya saa nne usiku Modessta Makote naye alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Alisema watoto wawili ambao ni Yona Sabuni na Cristina Yohana bado wamelazwa katika Hospitali Teule ya Mkoa wa Katavi wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri .
Aidha baada ya tukio hilo timu ya madaktari walifanya uchunguzi wa kitabibu katika miili ya marehemu wote watatu na baada ya uchunguzi kukamilika ilikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwajili ya taratibu za mazishi .
Kamanda Kuzaga alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote anaeshikiliwa na jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo.
Alisema uchunguzi bado unaendelea kufanyika kuhusiana na tukio hili ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini aina ya sumu iliyosababisha vifo vya watoto hao .