31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Watoto wanaokua haraka wako hatarini kupata kibiongo

Mchoro unaoonyesha uti wa mgongo uliopinda
Mchoro unaoonyesha uti wa mgongo uliopinda

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WAPO watu wazima ambao leo hii tunaishi nao kwenye jamii zetu wakiwa na ulemavu wa kupinda mgongo (Kibiongo).

Lakini wengi huwa hatujui sababu zilizochangia wenzetu hao kuwa katika hali hiyo ya kupinda mgongo.

Wataalamu wanaeleza kwamba tatizo hilo huwakumba wengi wakiwa katika umri wa utoto lakini kutokana na kutogundulika mapema huonekana wakiwa tayari wamekuwa watu wazima.

DAKTARI

Daktari Bingwa wa Watoto katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Bryson Mcharo, anasema hali hiyo hutokana na watoto kuzaliwa na mishipa laini ya uti wa mgongo.

“Tatizo la kupinda mgongo kitaalamu linajulikana kama ‘Scoliosis’, baadhi ya watoto huzaliwa na mishipa laini kwenye uti wa mgongo, sababu hasa inayosababisha hali hiyo bado haijulikani hadi hii leo.

“Lakini kwa wanawake wanasema huchangiwa na mfumo wao wa homoni, watoto wanaokua haraka kuliko umri wao huwa kwenye hatari ya kupata tatizo hili pia baadae ukubwani,” anasema.

Dk. Mcharo anasema kwa asilimia 30 tatizo la kibiongo hurithiwa toka kizazi kimoja hadi kingine ndani ya familia.

“Ndio maana unaweza kukuta kwa mfano baba ana kibiongo na watoto wake kadhaa wanakuwa wamezaliwa na tatizo, ni tatizo ambalo linarithiwa ndani ya familia,” anasema.

DALILI ZA MTOTO MWENYE KIBIONGO

Daktari huyo anasema tatizo hilo si rahisi kuligundua lakini linaweza kutambulika kwa kufanya vipimo vya kimaabara.

“Japo si rahisi kulibaini lakini wazazi wajenge utamaduni wa kuwakagua watoto wao sehemu za mgongoni, iwapo wataona uti wa mgongo unachora alama C au S ni vema wawalete hospitalini ili tuwafanyie uchunguzi zaidi,” anasema Dk. Mcharo.

Anasema iwapo uti wa mgongo wa mtoto unachora alama C au S si ishara nzuri na kwamba asipopatiwa matibabu ya mapema mgongo wake huishia kupinda yaani kibiongo.

“Hapa MOI tuna kliniki ya watu wazima wenye matatizo ya maumivu ya mgongo, lakini tunaona wanaletwa na watoto, tumegundua kwamba wengi wamezaliwa na tatizo hili lakini bado hawaletwi hospitalini.

“Nadhani ni kwa sababu bado jamii haijapewa elimu ya kutosha kwamba ugonjwa huu unatibika kwa kufanya upasuaji, katika kliniki yetu tunaona watoto wawili kila wiki wanaoletwa kupata matibabu,” anasema.

SIMULIZI YA MGONJWA

Vivian Kimondo (13), wakati akiwa na miaka 11 aligundulika kuwa uti wake wa mgongo una kasoro.

Itika Mwankenja ambaye ni mama mzazi wa Vivian anasema, mtoto wake huyo ni wa pili kuzaliwa akiwa na pacha wake lakini wenzake wote hawana tatizo hilo.

“Vivian ana pacha wake ni uzao wangu wa pili, wenzake hawana tatizo hata yeye alizaliwa salama, lakini siku moja alipokuwa akifua nguo zake wenzake walishangaa kuona mgongo wake ukiwa umechora alama S.

“Sikuwepo nyumbani siku hiyo, niliporejea walinieleza na familia yangu waliona si hali ya kawaida mgongo kuchora namna ile wakanishauri nimfikishe hiospitalini kwa vipimo zaidi,” anasema Mwankenja.

Anasema alimfikisha MOI ambapo madaktari wakamfanyia vipimo lakini hawakugundua chochote.

“Nilirudi nyumbani ila ilipofika mwaka huu, ile alama ya S ilizidi kuonekana na mgongo wake ukawa umepinda waziwazi, nikamrudisha hapa hospitalini baada ya madaktari kumpima kwa CT-Scan ndipo wakaona uti wake wa mgongo una tatizo.

“Wakaniambia kwa hali ilivyofikia alitakiwa kusafirishwa kwenda India kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kunyoosha mgongo, niliogopa mno kusikia hivyo,” anasema.

Anasema hakuwa na jinsi zaidi ya kumuomba Mungu kwamba watakapoenda nchini humo madaktari waweze kufanya upasuaji huo kwa ufanisi.

“Lakini kabla tarehe ya safari haijafika daktari wake aliniambia kwamba hatasafirishwa tena na badala yake upasuaji huo utafanyika hapa MOI, namshukuru Mungu tangu amefanyiwa Oktoba 5 mwaka huu,  hali yake inaendelea vema,” anasema.

Mtoto huyo anasema anapenda aje kuwa daktari katika maisha yake ili naye aweze kuisaidia jamii kutibu maradhi mbalimbali yanayowatesa watu wengi.

UPASUAJI GHALI

Kaimu Mkurugenzi wa MOI, Dk. Othuman Kiloloma, anasema wamefanikisha upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari bingwa wenzao kutoka Hospitali ya COEDN (Children Orthopaedic for Education Development Nation) iliyopo nchini Marekani na Chuo cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (COSECSA).

“Ni upasuaji ghali, kila mwaka tulikuwa tunapeleka watoto kati ya 15 hadi 20 nchini India kufanyiwa upasuaji huu na kila mtoto alikuwa akilipiwa na serikali kati ya Dola 60,000 hadi 80,000.

“Kwa fedha yetu ya Tanzania hizo ni sawa na Sh milioni 250 hadi 300 ambazo zilikuwa zikitumika kwa kila mtoto mmoja, hivyo hali hii naweza kusema kwa namna moja au nyingine ndiyo iliyokuwa ikisababisha deni kuongezeka.

“Lakini sasa tutakuwa tunafanya hapa hapa MOI, COSECSA na COEDN. Kwa huyu mtoto mmoja tumetumia Sh milioni tatu pekee na hizo zilitumika kununua vifaa ambavyo tumemuwekea kwenye uti wake wa mgongo ili uweze kunyooka,” anasema.

Anasema kuanza kutolewa matibabu hayo nchini kutaiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika nje ya nchi na kuokoa maisha ya watoto wengi.

MOI KUFANYA UPASUAJI

Dk. Kiloloma anasema wameanzisha kozi ya upasuaji wa mifupa ya uti wa mgongo uliopinda hospitalini hapo na kwamba hatua hiyo itaifanya MOI kuwa kitovu cha mafunzo na matibabu hayo Afrika Mashariki.

“Walimu hawa kutoka nje ya nchi watafundisha ndani ya hospitali yetu na kuzalisha wataalamu wengi zaidi, haya ni manufaa kwa nchi yetu ambapo sasa tunajivunia kwani tunakuwa kitovu cha matibabu na mafunzo Afrika Mashariki,” anasema Dk. Kiloloma.

USHAURI

Dk. Kiloloma anaishauri jamii hasa familia ambazo zina watoto wenye tatizo la kupinda mgongo kuwafikisha hospitalini hapo ili wapate matibabu.

“Mtoto akiwahishwa hospitalini matibabu yake ni rahisi zaidi kuliko akiwa tayari amekuwa mtu mzima, ingawa wapo wanaozaliwa na mifupa laini lakini wapo wengine ambao hupata tatizo baada ya kuugua magonjwa mbalimbali ikiwamo Kifua Kikuu (TB) au kupata maambukizi ya magonjwa kwenye uti wa mgongo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,581FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles