25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Watoto walia wakitoa ushahidi baba wa kambo alivyomuua mama yao

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

WATOTO, akiwamo mmoja wa miaka 10, wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, walivyoshuhudia baba yao wa kambo, Godfrey Nkwambi, akimnyonga mama yao Bahati Hussein.

Watoto hao, huku wengine wakibubujikwa machozi, walitoa ushahidi huo jana katika kesi ya mauaji inayomkabili Nkwambi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Msajili Pamela Mazengo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Erick Shija, mtoto mwenye umri wa miaka 10, alidai yeye hulala chumbani kwa mama yake chini kwenye godoro pamoja na mdogo wake wakati mama yake na baba huyo hulala kitandani.

“Siku hiyo usiku nilishtuka nikamuona Godfrey akimnyonga mama na aliniambia nisipige kelele na mama yangu alikuwa akitikisa miguu huku akitoa sauti kwa mbali.

“Nilimuona Godfrey akifanya hivi alafu hivi (akionesha hakimu huku mikono yake ikiwa imeshika kichwa na kidevu na kujizungusha), mama alikuwa akipiga miguu kitandani na kutoa kelele kwa mbali, God akanambia nisipige kelele, mimi nikanyamaza, nikamuona God akitoka nje, sikujua kilichoendelea kwani niliendelea kulala hadi asubuhi.

“Asubuhi nilimuacha mama yangu akiwa bado amelala, nikatoka  nje kusafisha meno nikaenda kucheza,” alidai.

Shahidi huyo alidai siku hiyo hakumuona Godfrey na hakujua alipokwenda na baadaye alisikia watu wakilia nyumbani kwao na ndipo ndugu zake walipomwambia kuwa mama yao amefariki.

Mtoto mwingine wa marehemu mwenye miaka 15, alidai  mama yake alifariki Juni 21, mwaka 2014 ambapo Juni 20 mwaka huo alipotoka kucheza alikuta baba yake (mshtakiwa), mama yake na watu wengine wakiwa wamekaa katika mkeka nyumbani kwao Ulongoni.

“Dada yangu, aliniambia kulikuwa na ugomvi kati ya baba na mama yangu ambao ulisuluhishwa na kwisha na baadaye nilimshuhudia (baba) mshtakiwa akimpa fedha mama  akanunue mboga kwa ajili ya chakula cha usiku.

“Saa 5 usiku nilienda kuwalaza wadogo zangu chumbani kwa mama na mimi nilienda kulala chumbani kwangu na mtoto wa mama mdogo.

“Usiku nilishtuka nikasikia mama na Godfrey wanagombana, mtoto wa mama mdogo alikuwa anaogopa, nikamwambia yataisha sisi tulale, tukabaki macho kitandani, mtoto wa mama mdogo akabanwa na haja ndogo, hivyo tukatoka nje kujisaidia,” alidai.

Alidai walipotoka nje walimuona Godfrey akiwa amekaa katika kochi sebuleni akiwa amevaa kipensi, shati begani huku akimiminikwa na jasho na kuwahoji wanapokwenda.

“Sisi tulimjibu tunaenda kujisaidia, akasema haya, tuliporudi tukasikia Godfrey akifungua mlango wa sebuleni na kutoka nje, sisi tulijificha nyuma ya mlango wa sebuleni, tulimsikia Godfrey akimgongea mpangaji wa chumba cha nje na kumuuliza kama alisikia kelele, yule mpangaji akamwambia hakusikia kelele,” alidai shahidi.

Alidai baadae walienda kulala, asubuhi aliamshwa na mama mwenye nyumba ambaye alimtaka achukue beseni la vyombo apeleke chumbani kwa mama yake.

Huku akitokwa na machozi, shahidi huyo alidai aligonga mlango, lakini mama yake hakuitikia na alipoingia ndani alimkuta mama yake amelala, akiwa amefunikwa shuka jeupe na kanga kichwani, alimtikisa hakuamka na akatoka nje akipiga kelele.

“Nilikuta mama kalala, niliendelea kumwamsha bila mafanikio, nikamfunua alikuwa hajavaa nguo, nikamshika kifua kuona kama roho yake inadunda, ilikuwa haidundi, nikatoka nje nikipiga kelele, mama mwenye nyumba aliniuliza nikamwambia mama yangu ahemi amefunikwa nguo, majirani walikuja na kumwangalia, wakasema atakuwa amezimia, wakamvalisha nguo na kumpeleka hospitali.

“Watu waliorudi hospitali waliniambia kuwa mama amekufa na alinyongwa, mama alinyongwa na Godifrey kwa sababu alishawahi kumtamkia kuwa atamuua yeye na familia yake kwani hataki kuiona.

“Mama pia alishawahi kunambia kwamba, ‘mwanangu nikifa Godfrey ndio kaniua’,” alidai.

Mtoto mwingine ambaye alikuwa akimwita marehemu shangazi, aliieleza mahakama kwamba wawili hao walikuwa na ugomvi na kuwa Godfrey alikuwa akimtuhumu Bahati kuwa na mahusiano ya kimapenzi na jirani yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles