Na Amina Omari, TANGA
JESHI la Polisi mkoani Tanga, limewakamata watu 125 wanaodaiwa kujiita watoto wa ibilisi ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Akizungumzia na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema watu hao wamekamatwa kutokana na operesheni inayoendeshwa na jeshi hilo maeneo mbalimbali.
Alisema watuhumiwa wamekamatwa wakituhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya uhalifu, ikiwamo wa kutumia silaha .
“Tumeweza kukamata silaha za moto tatu na risasi 11,kilo 11.05 za dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi kilo 36, pombe haramu ya gongo lita 239 na pikipiki 9 ambazo zinatumika katika matukio ya uhalifu,”alisema.
Kuhusu wananchi kukaribisha mwaka mpya, Kamanda Bukombe alisema jeshi hilo limepiga marufuku urushaji wa baruti na uchomaji wa matairi barabarani.
Alisema ili kudhibiti vitendo hivyo,jeshi hilo litahakikisha wanawachukulia hatua kali watu wote watakaohusika na kuchoma matairi na milipuko .
“Tumeweza kutoa vibali vya kurusha fataki, hatutashindwa kuwachulia hatua kali wale ambao watatumia sherehe hizo kufanya vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa kuchoma matairi na milipuko “alisema.
Aliwataka wananchi kusherehekea vizuri mwaka mpya bila ya kukiuka taratibu za kisheria kwa kufanya vurugu.