25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Watoto 994,109  kupatiwa chanjo ya polio Mwanza

*Ni kupitia kampeni ya chanjo ya kuzuia ugonjwa huo awamu ya tatu

Na Clara Matimo, Mwanza

Jumla ya watoto 994,109 wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Mwanza wanatarajia kupatiwa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio katika kampeni ya awamu ya tatu ya kukabiliana na ugonjwa huo.

 Hayo yamebainishwa  na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima leo Agosti 31, 2022 wakati akitoa taarifa ya mkoa huo  kuhusu kampeni ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio kwa waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema Kampeni hiyo ya awamu ya tatu itaanza Septemba Mosi hadi 04,2022,  itafanyika kwa kupita nyumba kwa nyumba na kwenye maeneo maalumu ikiwemo standi  huku akitoa rai kwa wazazi na walezi wote wenye watoto walio na umri chini ya miaka mitano kuwaandaa watoto wao ili waweze kupatiwa chanjo hiyo muhimu kwa ustawi wa afya na makuzi yao.

Aidha mkuu huyo wa mkoa amewasihi wananchi wote mkoani humo wawe mabalozi kwa kuwahamasisha wazazi na walezi wenye watoto walio na umri chini ya miaka mitano ili watoto wao wapatiwe chanjo hiyo ambayo ni ya matone na itatolewa kupitia mdomoni waweze kuwaepusha watoto hao na madhara yatokanayo na ugonjwa huo.

“Na nyie waandishi wa habari muwahamasishe wazazi na walezi walio na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili wahakikishe watoto wao wanapata chanjo ya polio vilevile  nyie waandishi wa habari kama mna watoto wenye umri huo hakikisheni watoto wenu nao wanapata chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio kwani ugonjwa huo unapompata mtoto unamfanya akose haki zake ikiwemo kucheza.

“Naomba wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza na nyie waandishi wa habari wote kwa pamoja tushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na ogonjwa huu kwa watoto wetu, Mungu asaidie watoto wote wapate chanjo ili wasipate maambukizi ya ugonjwa huo maana ni ugonjwa hatari sana kwa watoto husababisha baadhi ya viuno kulegea au kupooza sehemu mbalimbali za mwili,”amesema Malima.

Malima amefafanua kwamba mkoa wa Mwanza umepokea jumla ya dozi 1,040,000 za chanjo ya polio na tayari zimeishasambazwa katika halmashauri zote nane zilizopo mkoani humo pamoja na kwenye vituo vya huduma.

“Jumla ya timu 2,308 zenye jumla ya watumishi 6,924 zitatumika kutoa chanjo za polio awamu ya tatu na kila timu moja itakuwa na watumishi watatu ambao ni mchanjaji, mtunza takwimu na mhamasishaji hivyo wazazi na walezi wasihofu watakapofikiwa na watumishi hao lengo la serikali ni kuhakikisha tunakabiliana na ugonjwa huu ambao ulitokea nchi jirani za Malawi na Msumbuji,”amesema.

Malima amesema kupitia kampeni ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio awamu ya pili iliyofanyika Mei 18 hadi 21, mwaka huu jumla ya watoto 965,229 sawa na asilimia 114 kati ya watoto 846,773 waliolengwa walipata chanjo hiyo ambapo halmashauri zote nane za mkoa huo zilifanikiwa kuvuka lengo lililokuwa limewekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles