22.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Watoto 57 wenye ulemavu waomba msaada wa baiskeli

Na ELIUD NGONDO

-MBARALI

ZAIDI ya watoto 57 wenye ulemavu wa viungo wilayani Mbarali mkoani Mbeya, wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kuwasaidia kupata baiskeli ili kurahisisha kutokutembea umbali mrefu wakiwa wanakwenda shule pamoja na kuondokana na changamoto nyingine.

Akizungumza jana kwa niaba ya watoto wenzake, mtoto Faraja Msigwa (12), alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi, na kubwa zaidi ni ukosefu wa baiskeli ambazo zingeweza kuwapatia fursa ya kupata huduma ya elimu kama watoto wengine wasio na changamoto hiyo ya ulemavu.

Alisema ukosefu wa vifaa hivyo umekuwa ni changamoto kubwa kwao, hivyo kuwafanya kuishi kwa shida kulingana na mazingira waliyonayo.

 “Tunaomba Serikali na wadau mbalimbali watusaidie juu ya suala hili kwani tumekuwa tukiteseka sana sisi watoto wenye ulemavu, pili kutokana na hili tunakosa hata fursa ya kupata elimu kama wenzetu ambao hawana changamoto yoyote ya ulemavu,” alisema Faraja.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Child of Tanzania, Dafroza Mbota, alisema kutokana na kuwepo na changamoto kubwa ya watoto wenye ulemavu wilayani hapa, waliamua kuanzisha shirika kwa lengo la kuwawezesha kupata elimu.

Mbota alisema licha ya kituo hicho kuendelea kutoa elimu kwa jamii na kuwakusanya watoto wenye ulemavu kukaa sehemu moja, bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya baiskeli za walemavu na usafiri wa gari ya kuwafikisha kituoni waweze kusoma.

Alisema kutokana na umuhimu huo, wazazi na walezi wanatakiwa kuwapeleka watoto wenye ulemavu katika vituo vya kulelea yatima ili wapate mahitaji kuliko kuwaficha ndani na wengine waachane na imani potofu kuwa kuzaa watoto wenye ulemavu ni mkosi.

Kwa upande wake, Ford Mickson, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, alisema changamoto za watoto hao zitafanyiwa kazi kwa kushirikiana na kituo hicho na wadau mbalimbali ili kuhakikisha zinatatuliwa.

 “Changamoto kubwa kwa watoto wengi ni ukosefu wa baiskeli za walemavu kama walivyoeleza, ili watoto hao waendelee kusoma na kupata mahitaji mbalimbali, ipo haja Serikali na wadau kuona umuhimu wa kuwapatia baiskeli watoto hawa,” alisema Mickson.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles