NA VERONICA ROMWALD
WATOTO 24 waliozaliwa na matatizo ya usikivu (viziwi) watafanyiwa upasuaji wa kupandikizwa vifaa vya usikivu kila mwaka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema hayo mwishoni mwa wiki alipozungumza na MTANZANIA.
“Hii ni huduma mpya ambayo Muhimbili tumeianzisha na ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
“Tumepanga kila mwaka kufanya upasuaji katika awamu nne, kila robo tatu ya kwanza ya mwaka tutawafanyia watoto sita,” alisema.
Alisema tayari katika robo tatu ya kwanza ya mwaka, Aprili hadi Juni, wamefanyiwa upasuaji watoto sita kwa mafanikio makubwa.
“Watoto hao wanaendelea vizuri baada ya upasuaji, sasa hivi madaktari wanaendelea kutoa huduma za kliniki kama kawaida na kufuatilia hali zao.
“Hivyo watapanga tena orodha nyingine ya watoto ambao watafanyiwa upasuaji katika awamu inayofuata,” alisema.
Inakadiriwa kila mwaka watoto 200 huzaliwa na tatizo la usikivu na hivyo kuhitaji upasuaji awali walikuwa wakipewa rufaa kwenda India kupata huduma hiyo ya upasuaji.
Tangu mwaka 2003 hadi sasa wagonjwa 50 pekee ndiyo walionufaika na mpango wa ufadhili wa serikali.