Na Nyemo Malecela, Kagera
WATOTO 224,364 sawa na asilimia 39.8 wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Kagera wanakabiliwa na utapiamlo.
Kufuatia kuwepo kwa idadi hiyo kubwa ya watoto wenye utapiamlo mkoani Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo amesema Wataalam wa lishe mkoani Kagera wanatakiwa kuangalia upya na kutathimini ni wapi Mkoa huo unapokosea.
Kinawilo ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 11, alipokuwa akizungumza na wataalamu hao wa lishe mjini Bukoba.
“Tutazame upya na kutathimini ni wapi Mkoa unapokosea, tatizo liko wapi? kama vyakula tunavyo vya kutosha, labda hatujui namna ya kuvitumia, wazazi hawafahamu namna ya kulisha familia zao ili tuanzie hapo kurekebisha kasoro tulizonazo zinazopelekea kuwa na idadi kubwa ya utapiamlo.
“Pia tuchukue hatua mapema kwa watoto wanaozaliwa kuanzia sasa, tuainishe mikakati ya kuzifikia familia wanakozaliwa watoto kuanzia sasa ili kuwapa elimu wazazi ya namna gani ya kuwasaidia watoto hao wasipate utapiamlo,” amesema Kinawilo.
Kinawilo amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kutumia vizuri mvua za masika kuzalisha mazao yatakayosaidia kuondoa udumavu na kutuongezea kipato.
“Tunaweza kulima mahindi kwa lengo la kuuza na kuongeza kipato cha familia kitakachotuwezesha kununua vyakula mbadala kwa kuwa wenyeji wa Bukoba hawapendi kula ugali.
“Mahindi yana soko kwenye nchi zote zinazoizunguka Tanzania lakini tukumbuke swala la luna she ni swala nyeti, wataalam na viongozi wanatakiwa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa ili kushusha kiwango cha utapiamlo mkoani Kagera,” amesema Kinawilo.
Naye, Sued Rashid ambaye ni Msimamizi wa wahudumu wa afya Bukoba Vijijini amesema katika afua za lishe wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi wanapoihudumia jamii.
“Changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa kukusanya vyakula vinavyopatikana katika mazingira wanayoishi na kuviunganisha kwenye makundi makuu matano ya vyakula.
“Pia ushiriki wa wanaume katika masuala ya lishe katika familia ni mdogo jambo ambalo linasababisha wanawake kukabiliwa na majukumu makubwa yanayowanyima muda wa kuwahudumia watoto na familia inavyotakiwa,” amesema.
Alisema mwanamke huyo anashindwa kuelewa ni muda gani anatakiwa aandae chakula kwa wakati, mtoto apewe chakula mara ngapi kwa siku.
“Mwanamke anaweza kuwa anajua namna ya kuandaa chakula cha mtoto kwa kuzingatia makundi matano ya chakula ila akawa hajui anatakiwa kumpatia mtoto huyo chakula hicho mara ngapi kwa siku na kati ya mlo na mlo mtoto anatakiwa kula nini wakati huo akawa hazingatii suala la usafi jambo ambalo bado linaweza kuchangia utapiamlo kuendelea kuongezeka,” alisema Rashid.