29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto 115 wanaswa wakipatiwa mafunzo Dodoma

Na Debora Sanja, Dodoma

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limeviweka chini ya ulinzi na kuvifanyia uchunguzi vituo vitatu vilivyokusanya watoto 115 kutoka mikoa 13 nchini kwa lengo la kuwapatia mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Vituo hivyo vyote vipo katika eneo la Nkuhungu, lililopo katika Manispaa ya Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema wanafanya uchunguzi katika vituo hivyo kutokana na kuhusika kuendesha vituo vya kulelea watoto bila kusajiliwa na hatarishi.

“Jana (juzi) saa sita usiku tulifanya upekuzi katika vituo vitatu, katika kituo cha kwanza tukafanikiwa kukuta watoto takribani 63, kati yao 46 chini ya miaka 18.

“Katika kituo cha pili tulikuta watoto 40, kati yao walio chini ya umri wa miaka 18 walikuwa 12, kituo cha tatu tuliwakuta watoto saba, kati yao wenye umri chini ya 18 ni watano,” alisema Misime.

Alisema katika idadi ya watoto wote hao, 63 wana umri wa chini ya miaka 18 na wengine 52 umri wao ni miaka 25.

Alisema watoto hao wote ni wanaume na wengi wanatoka katika Wilaya ya Kondoa ambao ni 50 na watoto 26 wanatokea katika Wilaya ya Dodoma Mjini, Chamwino na Mpwapwa.

“Watoto wanaosalia wanatokea mikoa ya Kagera, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Zanzibar, Tanga, Tabora, Singida, Pwani, Lindi, Mtwara, Geita, Mwanza na Manyara,” alisema Misime.

Alisema watoto hao walikutwa usiku wakiwa wamechanganywa bila kujali
umri wao, jambo ambalo ni hatarishi.

“Uchunguzi unaendelea na yeyote atakayeguswa na ushahidi kuwa amekiuka
sheria atafikishwa mahakamani, ikiwepo wazazi walioruhusu watoto hao kuwa katika uangalizi ambao si wa kutosha kama Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inavyoelekeza,” alisema Misime.

MTANZANIA Jumamosi jana ilifika katika moja ya nyumba hizo ambayo iko eneo la Nkuhungu CCM katika Manispaa ya Dodoma inayohifadhi watoto takriban 60 na kushuhudia watoto hao wenye umri kuanzia miaka mitatu na kuendelea wakiendelea na shughuli zao na wengine wakinywa uji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya majirani walisema wameanza kuwaona watoto hao tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Mmoja wa jirani hao, Mama Naomi, alisema siku zote amekuwa akiwaona watoto hao wakishinda hapo na hajawahi kuwaona wakienda shule kusoma.

“Chakula na kuni za kupikia huwa wanaletewa na walimu wao, wanajipikia wenyewe, wale watoto wadogo kazi yao ni kuosha vyombo,” alisema Mama Naomi.

Wakizungumza katika eneo hilo, baadhi ya watoto hao walisema wapo hapo kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Walipoulizwa kama wanaenda shule kutokana na wao kuwa na umri mdogo, watoto hao walijibu kuwa baadhi yao wanasoma elimu ya msingi na wengine sekondari.

“Mimi nimetoka Kondoa lakini nilipokuja hapa nimeandikishwa Shule ya Msingi Nkuhungu, nikimaliza kusoma dini hapa huwa nakwenda shuleni,” alisema mmoja wa watoto hao.

Akizungumzia tukio hilo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajab, alisema hakuna dhambi yoyote kwa watoto hao kulelewa katika kituo hicho.

“Hayo ni mafunzo katika madrasa ambazo zilianza zamani ulimwenguni kote, polisi haina mamlaka ya kufunga madrasa, labda kama watakuta kuna tatizo lolote la kuhatarisha amani,” alisema Rajab.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Betty Mkwasa, alisema amesikitishwa na hali ya mazingira katika eneo hilo ambayo hayafai kuishi binadamu wa kawaida
na kuahidi Serikali itachukua hatua za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles